Ruto Alia Hujuma Kupanda Bei Ya Mafuta ya Petroli

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ameipa changamoto Serikali kutoka hadharani na kueleza chanzo cha alichokiita “mgogoro wa kutengeneza” kuhusu kupaa bei ya mafuta ya petroli na dizeli.

Ruto amesema kinachoitwa uhaba wa mafuta sasa hivi ni mpango wa genge la vigogo serikalini wanaotaka bei ya nishati hiyo kupanda kwa masilahi yao binafsi.

Akiwa nyumbani kwake, Karen, Nairobi, Ruto aliwaambia waandishi wa habari kuwa kupanda kwa bei ya mafuta Kenya hakuna uhusiano na mgogoro wa mafuta duniani.

Hivi karibuni, Ruto akiwa kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni za urais, alisema kwa nafasi yake kama Naibu Rais, hakuna siri wala mfumo ambao haujui.

“Kupanda kwa bei ya mafuta kwa sasa ni matokeo ya ushirikiano kati ya genge la wachache wanaohodhi biashara ya mafuta na maofisa wa Serikali wanaohujumu uchumi. Upande mwingine ni matokeo ya kuwa watumishi wa umma wazembe, wasiojali na wasio na uwezo,” alisema Ruto.

Alisema kuwa kwa sasa mamlaka za nchi zimezungukwa na watu wenye mgongano wa masilahi na wanaotaka kujichotea mali za umma. Ruto alisema watu wa aina hiyo wamezunguka sekta zote za uchumi Kenya.

“Uchu wa kujitajirisha binafsi na rushwa ni mambo ambayo yanatupeleka kwenda kuanguka kwenye bonde kali. Wakenya wanataka haya mambo ya mgongano wa masilahi yafike ukomo,” alisema Ruto.

Ruto alihoji zilipo fedha za Kenya Sh39 bilioni (Sh720 bilioni) za Mfuko wa Maendeleo ya Petroli zenye lengo la kusaidia upatikanaji wa mafuta na kupoza bei. Alisema, Serikali ilibadili matumizi ya fedha hizo na kuzitumia kuhudumia mikopo na kujenga miundombinu ya maendeleo bila kupata kibali cha Bunge.

Ruto aliitaka Wizara ya Nishati kuweka wazi taarifa jinsi mafuta yaliyoingia Kenya yalivyogawanywa kwa wauzaji wa mafuta katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Muswada wa Bidhaa za Petroli wa mwaka 2021, pamoja na mabadiliko ya kodi na tozo zake, ambao ulikwamishwa, unatakiwa kuingizwa kwenye mchakato katika hali ya dharura ili kusaidia kushughulikia tatizo la uhaba wa mafuta,” alisema Ruto.

Katika mkutano huo, Ruto aliongozana na Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi, aliyekuwa kiongozi wa kambi ya wabunge walio wengi, Aden Duale na Seneta wa Nakuru, Susan Kihika.

Ruto alisema, nchi nzima inapitia maumivu ya jumla ya anguko la kiuchumi, akaongeza kuwa watu wachache ambao wananufaika na tatizo la kutengeneza la uhaba wa mafuta ndio wanaosababisha kupaa kwa bei ya mafuta.

“Mamilioni ya Wakenya wanashuhudia wakiwa wamechanganyikiwa na wanaumizwa jinsi vituo vya mafuta vinavyokaukiwa, foleni zinakuwa kubwa kupata huduma kwa sababu ya hili tatizo la kutengeneza, ambalo kwa kiwango kikubwa limeivuruga sekta ya usafirishaji.

“Wakenya sasa hivi wanalazimishwa kutoa zaidi kutoka kwenye mifuko yao ili kupata mafuta, hata kulipa nauli za basi. Madereva wa bodaboda wanashindwa kufanya kazi kwa sababu kupanda kwa bei ya mafuta. Kupanda bei ya chakula kumesababisha gharama za maisha kupanda kwa kiasi kikubwa na kuumiza mamilioni ya Wakenya,” alisema Ruto na kuongeza:

“Wakulima wengi wameshindwa kupanda mazao kwenye mashamba yao kwa sababu ya kushindwa kumudu bei ya mbolea ambayo imepanda juu mno. Mfuko wa mbolea wa kilo 50 uliokuwa unauzwa Sh3,000 (Sh60,000 za Tanzania), hivi sasa unauzwa Sh7,000 (Sh140,000 za Tanzania).”

Wakati Ruto akiyasema hayo, wiki iliyopita Waziri wa Kilimo nchini Kenya, Peter Munya alitangaza kushuka bei ya mbolea hadi kufikia Sh2,800 za Kenya, sawa na Sh56,000 za Tanzania kwa mfuko wa kilo 50.

Ruto anagombea urais kwa tiketi ya Kenya Kwanza Alliance, akikabiliana na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, ambaye anawania kuingia ofisi namba moja Kenya kwa leseni ya Azimio la Umoja.

Raila anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta, hivyo kumfanya Ruto kuwa kama mgombea wa upinzani.


Kwa nini Uhuru amembadilikia Ruto?

Kinachofahamika ni tofauti zilizojitokeza baada ya Uhuru na Raila kufanya mkutano Machi 2018, na kukubaliana kuzika chuki za kisiasa zilizoishika Kenya kwa miaka mingi.

Ruto aliununia mkono wa mapatano kati ya Uhuru na Raila, kwa kile alichodai kulikuwa na mambo mengi ya kuwafanyia Wakenya kuliko Uhuru kujielekeza katika kutengeneza suhulu na Raila.

Kisha, mkono huo ukazaa Mpango wa Kujenga Daraja (BBI), lengo likiwa kubadili sehemu kadhaa za katiba, ili kuzika chuki za kisiasa, vurugu za uchaguzi, siasa za ukabila na kuwezesha mgawanyo wa madaraka kwa vyama vinavyoshindwa uchaguzi.

Ruto alipinga hata maudhui ya BBI, akaeleza kuwa kila kitu kilichofuata baada ya mkono wa mapatano kati ya Uhuru na Raila, kilichelewesha mambo mengi ya msingi ambayo Serikali ilipaswa kuwatekelezea Wakenya.

Hivyo, kinachofahamika kwa wengi ni kuwa Uhuru na Ruto wametofautiana kuhusu mapatano na Raila. Unaweza kusema kuwa Ruto alipata wivu wa kisiasa, kuona mshirika wake (Uhuru), anafanya maridhiano na hasimu wake katika uchaguzi unaokuja.

Kinachozungumzwa mtaani Kenya ni tofauti kuhusu mgogoro wa Uhuru na Ruto.

Kinachosemwa ni kwamba Uhuru amechagua kusimama na Raila kwa sababu wao wanatoka kwenye familia mbili ambazo zinaongoza kwa kujimegea vipande vikubwa vya keki ya taifa.

Uhuru ni mtoto wa Jomo Kenyatta, Rais Kwanza wa Kenya. Raila ni mwana wa Jaramog Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa Kwanza Kenya. Hivyo, wote wanatokea katika familia za viongozi wakuu waasisi wa Taifa la Kenya.

Katika hoja hii, Ruto pia anaitumia, na amekuwa akijenga hoja kuwa kumfanya Raila kuwa Rais wa Kenya baada ya Uhuru ni kuendeleza siasa za utawala wa kinasaba, hivyo Wakenya wanapaswa kumchagua yeye ili aingize vionjo tofauti vya uongozi.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments