Samia Afunguka Aliyopitia Royal Tour


 Rais Samia Suluhu Hassan amesema amejikuta akiendesha gari kwa mara nyingine wakati anarekodi filamu ya The Royal Tour iliyozinduliwa jana, tangu aache kufanya hivyo miaka 15 iliyopita.

Katika moja ya vipande vilivyoanza kusambazwa kwa matangazo kabla ya uzinduzi huo, Rais Samia alionekana akiendesha gari la utalii huku akizungumza na mtayarishaji wa kipindi hicho, Peter Greenberg.

Rais Samia alisema hayo alipokuwa akihojiwa na mtayarishaji wa filamu hiyo, Greenberg mbele ya umati wa waliohudhuria uzinduzi huo muda mfupi baada ya kuitazama usiku wa kuamkia jana.

Katika moja ya swali lake, Greenberg alimhoji kuhusu kipande cha video alichoonekana akiendesha gari kwamba ni muda mrefu hajafanya hivyo, Samia alijibu: “Ndiyo, ni tangu miaka 15 iliyopita.”

Rais Samia alitaja baadhi ya changamoto alizopitia wakati wa kurekodi filamu hiyo, ikiwamo vikwazo vya walinzi wake wakimtaka kuacha kufanya baadhi ya vitu.

“Ilikuwa ngumu ukizingatia nina walinzi wengi wanaoniambia usifanye hiki usifanye kile, usiende hapa usiende pale, ilhali nilipaswa kufanya, lakini nimefanikisha nashukuru Mungu,” alisema Rais Samia.

Katika filamu hiyo waliyoifanya kwa siku 14, Rais Samia alielezea baadhi ya siku walishindwa hata kupata mlo kwa wakati kutokana na kazi hiyo, akitolea mfano wakati wa kuingiza sauti.

“Unakumbuka siku tuliyokuwa tunaingiza sauti ‘Voice Over’ hatukupata mlo wa mchana na tulipata chakula cha jioni kwa kuchelewa, kwa hiyo siku nzima ilikuwa kwa ajili ya ‘Voice Over’ ulinitesa,” alisema na kuibua vicheko kutoka kwa waliohudhuria uzinduzi huo.

Hata hivyo, alisema kitu kikubwa ambacho Tanzania inajivunia ni ukarimu wa watu wake, “siku moja ukifika Tanzania hata kwa bahati mbaya, hutajutia.”

Alisema wakati anarekodiwa filamu hiyo hakutarajia kama ingeonekana kwa ukubwa unaoonekana sasa.

Alipoulizwa na mmoja wa wahudhuriaji kuhusu kipindi bora cha kutembelea Tanzania, alijibu Juni na Julai kwa kuwa sio msimu wa joto sana wala baridi.

“Lakini inategemea kama unataka kuona faru wanaohama katika hifadhi ya Serengeti unapaswa kuja Agosti, lakini vinginevyo, unaweza kuja muda wowote, tunaweza kusitisha mvua kwa ajili yako,” alizungumza kwa mzaha.

Mmoja wa waliohudhuria alitaka ushauri wake kwa mabinti juu ya kujiamini kwake, Samia alimjibu, “labda kitu ninachoweza kuwaambia mabinti ni kutambua wanataka kufanya nini, wanapaswa kujiamini, kusikiliza matamanio yao na kuhakikisha wanayatimiza, wanaweza kufika wanapotaka kwenda.”

Pia, alisema ana mpango wa kuwaunganisha waigizaji wa kike wa Tanzania na wengine wa kimataifa na tayari ameshakutana na kampuni kubwa tano za utalii.

“Tumezungumza mengi, lakini kampuni mojawapo inayofanya kazi na Paramount Film; tulikuwa na mazungumzo mazuri ya kuoanisha tamaduni za Tanzania na filamu zao, kwa hiyo nimeanza kufanyia kazi hilo,” alisema Rais Samia.

Muandaaji wa filamu hiyo, Greenberg alisema itarushwa katika mataifa yote duniani ikiwa na tafsiri za maandishi ya Kiswahili ‘subtitles.’

Uzinduzi huo unafuatiwa na utakaofanyika Los Angels Marekani, Aprili 21 kabla ya Dar es Salaam Aprili 28, kisha Zanzibar Mei 7, mwaka huu.

Filamu hiyo ilianza kurekodiwa Agosti 28, 2021 kwa siku 14, ikionyesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania.

Post a Comment

0 Comments