Sensa Kusaidia Kukabiliana Na Vitendo Vya Unyanyasaji-Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamisi


NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Ali Khamisi amesema kuna umuhimu mkubwa kwa watanzania  kujitokeza  kushiriki  zoezi la Sensa ya watu na Makazi kwa kuwa mbali na faida zingine pia itasaidia kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia nchini.

Ametoa rai wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kuwa kufanya hivyo kunasaidia  kuunga mkono juhudi zinazofaanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuiletea nchi maendeleo.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari Mwanaidi alisema ni muhimu kwa kila mtanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato huo ili kusaidia ukuaji wa maendeleo ya nchi kama ambavyo Rais Samia amesisitiza.

"Sensa ni muhimu, hauwezi kupanga maendeleo ya nchi kama hujajua idadi ya watu ulionao, Rais amesisitiza kuwa sote ni vyema tukajitokeza na kushiriki katika zoezi hilo Agosti 23 Mwaka huu, niwasihi tusimwangushe, tujitokeza kikamilifu" alisema Mwanaidi

Amesema kama Taifa kuna manufaa mengi ya kushiriki sensa hiyo, hivyo ni vyema kila mtu akaona umuhimu wake na kujitokeza siku hiyo kufanikisha suala hilo litakalotusaidia watanzania katika kujiletea maendeleo.

Mbali na hilo Mwanaidi pia alisema kwa kujitokeza kushiriki Sensa hiyo, kimsingi kutaiwesha Serikali hususani Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Waanawake na Makundi Maalumu  kutoa elimu ya ukatili  kijinsia uliopo katika nchini kwa urahisi na kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo.

Awali akizindua nembo ya sensa hiyo sambamba na tarehe ya kufanyika kwake, Rais Samia Suluhu Hassan alisesema zoezi hilo i muhimu kwa kuwa litaisaidia Serikali kuandaa sera na mipango mipya ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu na jinsi ya kuitekeleza na kufatilia utekelezaji wa mipango hiyo.

Alisema taarifa hizo zitakazopatikana kupitia zoezi hilo pia zitasaidia kujua wastani wa ongezeko la watu na hali ya uhamiaji mfano kutoka vijijini kuja mjini lakini hata waliotoka nje kuhamia na kuingia Tanzania.

"Sensa pia itatusaidia Serikali kufanya maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali za Taifa na kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, maji, umeme, ujenzi wa miundombinu kulingana na idadi ya watu na mahitaji ya maeneo hayo" alisema Rais Samia.

“Ili Sensa iweze kukidhi mahitaji ya kufanikisha malengo yote hayo ni lazima ishirikishe watu wote. Zoezi hili litakuwa ni kwa watu wote waliolala na kuamkia siku ya Sensa kwenye nchi ya Tanzania,” alisema Rais Samia.

Alisema licha ya uwepo wa tozo za makazi, Serikali haikuwa na idadi sahihi ya nyumba na makazi, hivyo zoezi hilo litatoa ubora kwa kujua anuani za makazi, idadi ya majumba na aina za nyumba zilizopo.
 Na Amiri Kilagalila

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments