Serikali Yaweka Msisitizo MSD Kununua Dawa Kutoka Viwandani

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema sheria ya manunuzi ya umma haijaweka kikwazo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani au kwa wazalishaji ili kushusha gharama za dawa.

Ummy ambaye ni mbunge wa Tanga Mjini amesema sheria hiyo imeweka mipaka sio tu gharama bali itaangalia ubora , ufanisi na upatikanaji wa dawa na kwamba utaratibu wa kununua dawa moja kwa moja umepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za dawa nchini.

Ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 13, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia  mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2022/2023 unaohitimishwa leo.

Katika maelezo yake,  Ummy amesema mwaka 2017 akiwa katika wizara hiyo Serikali iliingia mikataba na wazalishaji 73 na wazalishaji 46 wa dawa kutoka Uganda, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, Afrika ya Kusini, China, Falme za Kiarabu, Bangladesh, India, Kenya na Tanzania.

“Tulianisha aina za dawa 178, vifaa tiba 195 na vitendanishi 178. Hili suala sio geni limeshafanyika na lengo kushusha gharama ya dawa. Baada ya utaratibu kuanza kutumika dawa ya chanjo ya homa ya ini kabla ya kununua viwandani ilikuwa inauzwa Sh22, 000, sasa imeshuka hadi Sh 5,300."

“Dawa ya sindano kwa ajili ya maumivu vichupa 10 ilikuwa ikiuzwa Sh 2000, ikishuka hadi Sh 800, dawa ya kupambana na maambukizi ya bakteria miligramu 265 yenye vidonge 15 kwa wasambazaji  ilikuwa inauzwa Sh 9800 sasa imeshuka hadi Sh 4,000 na mashuka yalikuwa Sh 22,000 sasa Sh 11,000,” amesema.

Waziri Ummy amesema MSD kununua dawa moja kwa moja kutoka kwenye viwanda na wazalishaji ndio mwelekeo wa Serikali ili kushusha gharama za dawa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments