SIMBA SC YATHIBITISHA KUMKOSA MORRISON MCHEZO WA MARUDIANO DHIDI YA ORLANDO PIRATES FC

WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC wamethibitisha kumkosa Mchezaji wao raia wa Ghana, Bernard Morrison kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Orlando Pirates FC utakaochezwa nchini Afrika Kusini, Aprili 24, 2022.

Kupitia mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amesema Morrison atakosekana kwenye mchezo huo kutokana na hatosafiri na timu kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo huo utakaoamua hatma ya timu hiyo kufuzu hatua Nusu Fainali ya Michuano hiyo.

“Mchezaji Bernard Morrison atakosekana kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Afrika Kusini, kutokana na kuwepo na shida binafsi na Mamlaka ya Uhamiaji nchini humo”.

“Mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs hatukwenda naye, na mchezo huu dhidi ya Orlando Pirates FC hatutakwenda naye Afrika Kusini, badala yake katika mechi mbili atacheza mchezo mmoja pekee wa hapa nyumbani kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, majira ya Saa 1:00 Usiku”, amesema Ahmed Ally.

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Orlando Pirates FC, siku ya Jumanne, Simba SC itaanza rasmi Kampeni ya hamasa kuhakikisha Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo wanajitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo wa Robo Fainali, ambao Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limeruhusu Mashabiki Elfu 60 (60,000) kuingia uwanjani.

“Siku ya Jumanne tunaanza Kampeni rasmi tukipita kuhamasisha Mashabiki wetu kwa kuanzia Tawi la Simba Tunawakera, Chang’ombe Maduka Mawili, Temeke, Kigamboni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)”, ameeleza Ahmed.

Hata hivyo, Simba SC imekataa kutumia Tochi za kuwamulika Wachezaji wakiwa uwanjani badala yake imeruhusu kutumia Tochi za Simu binafsi sanjari na ‘Fire works’, Bendera, ‘Scarf’ za timu ili kuanikiza hamasa kwa Wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa nguvu na kupata ushindi dhidi ya Orlando Pirates FC.
Na Bakari Madjeshi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments