Uhuru Wa Habari Kuadhimishwa Katika Mazingira Tulivu Zaidi

Tanzania inatarajia kushiriki maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari unaoonekana kuongezeka baada ya kudumaa katika miaka mitano iliyopita.

Tanzania ilipitia wakati mgumu wa uhuru wa vyombo vya habari ikishuhudia baadhi vikifungiwa yakiwamo magazeti ya Tanzania Daima, Raia mwema, Uhuru, Mawio na Mwanahalisi, huku baadhi ya televisheni na vituo vya radio vikipigwa faini kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo, vyombo vingi vilivyofungwa vimefunguliwa ingawa vingi havijarudi hewani kutokana na changamoto za mtaji hata nguvukazi kwani wafanyakazi wengi walilazimika kutafuta shughuli za kufanya kipindi vimefungwa.

Mbali na hatua hizo, sheria kali zilipitishwa ikiwamo ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Utangazaji ya mwaka 2015 na Kanuni za Makosa ya Mtandaoni za mwaka 2015, na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2016 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau kwamba zinazkwaza uhuru wa habari nchini.

Katika maadhimisho ya mwaka huu ambayo kilele chake kitakuwa Mei 3 yakifanyika kitaifa jijini Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi akishuhudia wahariri na wageni kutoka nchi za Afrika Mashariki wakijadili namna ya kuiboresha sekta hiyo kuwa na mchango m kubwa zaidi katika ujenzi wa uchumi.

Maadhimisho hayo yatawakutanisha Jumuiya ya Wahariri wa Afrika Mashariki (EAES) na wadau wengine wa sekta ya habari barani Afrika kusherehekea na kujadili masuala ya uhuru wa vyombo vya habari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema ni jambo zuri na faraja kwa waandishi wa habari kwa Rais Samia kukubali kuwa mgeni rasmi katika siku hiyo muhimu.

“Kwa kweli tumefurahi sana kuona Rais anajumuika nasi siku ya maadhimisho ya vyombo vya habari na tunatarajia mengi kutokea katika sekta ya habari kuhakikisha upatikanaji wa uhuru wa habari,’’ alisema Meena.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliyoandaliwa na EAES alisema yanatarajia kujadili mambo mbalimbali yakiwamo masuala ya usalama wa wanahabari, tathmini ya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na changamoto katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika vyombo vya habari.

Pia utendakazi wa vyombo vya habari katika nyakati hizi za kidijitali na udhibiti wa faragha, ufuatiliaji wa mtandaoni na masuala ya udukuzi katika tasnia ya habari yatajadiliwa kwa kina ili kuwaongezea uelewa waandishi wa habari kabla hawajaujuza umma namna ya kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta tofauti ikiwamo Teknolojia ya Habarina Mawasiliano (Tehama).

Ofisa Habari Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Stella Vuzo alisema kufanyika kwa kongamano hili Tanzania ni fursa kwa wananchi kushirikiana kuona haki ya uhuru inapatikana kwa kuzingatiwa dhana za uandishi wa habari na kutoa changamoto kwa jamii.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments