UVCCM Yapata Makatibu Wa Wilaya Wapya

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umefanya uteuzi wa makatibu wa wilaya 168 kati ya hao zaidi ya 20 ni wapya.

Uteuzi huo ulifanywa na Sektarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa iliyoketi juzi Machi 30,2022 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention jijini Dodoma.

Akizungumza jana na Mwananchi Katibu Mkuu wa UVCCM Kenani Kihongosi alisema uteuzi huo unahusisha makatibu wapya zaidi ya 20.

“Wengine ni makatibu wapya, wengine ni wamehamishwa vituo vyao vya kazi na wengine wamebakia katika vituo vyao vya kazi,”alisema.

Uteuzi huo unafanyika wakati chama hicho kikiwa katika maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama utakaoanza katika ngazi ya matawi Aprili mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katiba wasimamizi wa chaguzi ndani ya UVCCM ni makatibu hao.

Akitoa maoni yake mmoja wa wanachama wa CCM, Amani Sefu alitaka waliopata nafasi hizo kufanya kazi kwa weledi na busara kwa kumtanguliza Mungu na maslahi ya Taifa.

“Hongereni sana wote mlioaminiwa mkatende kazi zenu kwa ufanisi mkubwa kwa kuwapigania vijana na chama kwa ujumla. Safi sana mmeaminiwa na chama. Kazi iendelee,”alisema.

Neema Nicodemus alisema uteuzi huo umekuja kwa wakati muafaka wakati chama kikiwa katika maandalizi ya uchaguzi ndani ya chama.

Aliwataka waliopata nafasi hizo kuhakikisha kuwa wanasimamia uchaguzi ndani ya chama kwa uadilifu mkubwa ili kuwapata viongozi bora wataokivusha chama katika chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2025.

“Uchaguzi (mkuu) hauko mbali, Uchaguzi wa ndani ya chama ni muhimu sana katika kukiwezesha chama kupata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu, wahakikishe wana usimamia kwa uadilifu ili kuhakikisha tunapata viongozi waliobora,”alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments