Vipigo kwenye ndoa tishio jingine kwa familia


 Wiki iliyopita simanzi iliwakumba watu wengi barani Afrika, hasa wafuatiliaji wa muziki wa injili baada ya kifo cha muimbaji wa nyimbo za injili Nigeria, Osinachi Nwachukwu (42) kilichodaiwa kuhusishwa na kipigo.

Muimbaji huyo alijizolea umaarufu kupitia wimbo wa Ekwueme alioshirikishwa na Mchungaji, Prosper Ochimana.

Binadamu wanasema kifo ni mipango ya Mungu. Licha ya usemi huo, kifo cha Osinachi kinaelezwa mumewe kudaiwa kuhusika kwa kiasi fulani kwa vipigo alivyokuwa akimpiga mama huyo.

Inadaiwa hata wakati mwingine watoto wake walikuwa wakishuhudia mama yao akipokea kipigo kutoka kwa baba yao na kulazimishwa kushiriki kumpiga.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya familia zinaeleza kuwa Osinachi amekuwa akivumilia ukatili aliokuwa akifanyiwa na mumewe akiamini ipo siku atabadilika, huku wachungaji wakitajwa kumshawishi kuendelea kuvumilia hata pale alipotaka kujaribu kuachana na ndoa hiyo.

Hali ilivyo kwa wanawake wengine

Kilichotokea kwa Osinachi kinaelezwa kuwakumba wanawake wengi walio kwenye ndoa au uhusiano.

Baadhi yao hujikuta wakivumilia vipigo na aina nyingine za ukatili kwa kuhofia kuwa wakipaza sauti uhusiano unaweza kuvunjika au watavuruga malezi ya watoto wao.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Wanawake Duniani (UN Women) mwaka 2020, wanawake 47,000 waliuawa na wenza au watu wa ndani ya familia.

Hii ni sawa na kila baada ya dakika 11 kuna mwanamke mmoja anapoteza maisha kwa sababu ya vipigo na ukatili kutoka kwa mwenza wake.

Pamoja na kukumbana na vipigo hivyo, lakini inaelezwa kuwa ni asilimia 40 pekee ya wanawake wanaotoa taarifa na kutafuta msaada, wengi huishia kunyamaza wakiamini mambo yanaweza kubadilika kadiri ya siku zinavyozidi kwenda.

Kati ya hao wanaotafuta msaada, wengi wanaishia kuzungumza kwa ndugu au marafiki na sio polisi au vituo vya afya kwa ajili ya kupata msaada wa kimatibabu.


Hali ikoje Tanzania

Hapa nchini ripoti ya Hali ya Haki za Binadamu ya mwaka 2021 inaonyesha vitendo vya ukatili wa wanawake majumbani vimeendelea kushamiri, huku ukimya ukitawala katika kutoa taarifa za vitendo hivyo kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki hii na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonyesha kwa mwaka jana pekee yalirekodiwa matukio 70 ya ukatili dhidi ya wanawake unaohusisha vipigo na mikoa iliyotajwa kutekeleza ukatili huo kwa kiwango kikubwa ni pamoja na Katavi, Kilimanjaro, Geita, Tabora, Shinyanga, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mara.

Asilimia 52 ya waliohojiwa kwenye utafiti huo wameeleza ukatili dhidi ya wanawake ni tatizo kubwa kwenye jamii wakati asilimia 41 wameeleza kuwa ni la kati.


Chanzo cha ukatili

Sababu kadhaa zilitajwa na waathirika wa vipigo hivyo, wivu wa mapenzi ulitajwa zaidi huku sababu nyingine zikiwa imani za kishirikina, kugombea haki ya usimamizi wa watoto, magonjwa na ulevi.

Umaskini na ukosefu wa kipato vimeendelea kuwa chanzo kikubwa cha ukatili dhidi ya wanawake, huku baadhi yao wakiwa hawana njia nyingine ya kukabiliana na vitendo hivyo na kuamua kuvumilia.

Wakati ripoti hiyo ikieleza hivyo, taarifa ya utafiti wa idadi ya watu na afya (TDHS), kwa mwaka 2015-2016 ilibaini kuwa asilimia 40 ya wanawake walioolewa wamewahi kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kijinsia au kihisia kutoka kwa wenza wao huku ikiweka wazi kuwa asilimia 39 ya wanawake wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili kama kupigwa na kuchomwa na vitu vyenye ncha kali.

Asilimia nne ya wanawake wamekatwa au kuchomwa kwa kusudi na wenza wao au wametishiwa au kushambuliwa kwa silaha mbalimbali, huku asilimia 36 ya wanawake wamewahi kufanyiwa ukatili wa kisaikolojia, mfano kutukanwa.


Simulizi ya mwathirika

Mariam Juma ni mfano wa wanawake waliolazimika kuacha ndoa zao kufuatia vitendo vya ukatili.

Licha ya kupigwa na kushambuliwa na vitu vyenye ncha kali mara kwa mara na mumewe, anaikumbuka siku ambayo mumewe huyo alimmwagia chai ya moto.

Akizungumzia namna alivyofanyiwa ukatili, alisema siku hiyo ndiyo ilikuwa hitimisho la safari yake ya ndoa iliyodumu kwa miaka mitano.

“Nilikuwa napigwa kwa muda mrefu, lakini kwa kuwa niliambiwa kwenye ndoa kuna mambo nivumilie, basi nikawa navumilia, mwili wangu wote ukawa na makovu yanayotokana na majeraha kama unavyoyaona mengine haya. Maana wakati mwingine nilikuwa napigwa na mikanda, chochote kilicho mbele yake alikitumia kunipigia, lakini nilivumilia na kujiuguza,” alisema Mariam.

“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nachemsha chai asubuhi, jana yake hakuwa amerudi nyumbani, aliporudi nikamuuliza amelala wapi, ndipo ugomvi ukazuka, kwa hasira akachukua ile chai iliyokuwa inachemka akanimwagia. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa uvumilivu wangu, niliondoka na kuanza kuchukua hatua kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika.”

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga alisema aina hiyo ya ukatili inaendelea kuwapo kwa sababu jamii inachukulia kama ni kitu cha kawaida, hivyo vipigo vinaendelea na kuwa sehemu ya maisha ya wanajamii wengi nchini.

“Unakuta mtu anapigwa na mume au mpenzi wake lakini anaona ni kitu cha kawaida, hii sio kawaida, kwanza inatakiwa hata akijaribu kukugusa kwa nia ya kukushambulia lazima ushtuke. Huu ukawaida ambao watu wanauchukulia husababisha wasitoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe na wachache wanaotoa huwa wanaishia njiani hawatoi ushahidi.”

Hilo linaelezwa pia na Julieth Andrea, anayesisitiza wanajamii kuwa mstari wa mbele kukemea na kuvitolea taarifa kwenye vyombo vya sheria vitendo vya aina hii.

Alisema kukaa kimya hadi mtu anapopoteza maisha ndiyo wazungumze wanachokifahamu si haki.

“Kilichotokea kwa Osinachi ni funzo kubwa kwa wanajamii, wapo waliokuwa wanafahamu magumu aliyokuwa anapitia, lakini hawakuthubutu kusema. Tukubaliane wanawake hawana nguvu wala uwezo wa kuamua kutokana na makuzi yao, hivyo wakati mwingine wanahitaji msaada wa nje,” alisema.

“Ifike mahali tuoneane huruma na kuguswa na shida za watu wengine, wengi wanapoteza maisha kwa mtindo huu wa vipigo na hata ukatili wa kisaikolojia, imetokea tumefahamu kuhusu Osinachi kwa kuwa yeye ni mtu maarufu.”

Mshauri wa Uhusiano, Deogratius Sukambi alisema tatizo hilo lipo kwa muda mrefu na linaendelea kukua huku akibainisha kuwa lina uhusiano wa moja kwa moja na afya ya akili.

Alisema tatizo hilo ni dosari za kihaiba au kiakili ambalo linamfanya mtu kuwa na tabia ya kutopenda kukosolewa au kupingwa mawazo yake.

“Watu wa aina hii mara nyingi wana haiba mbili, sura yake itaonekana mpole, mnyenyekevu, mwenye upendo lakini upande mwingine wana ukatili uliopitiliza. Ukikaa na mtu kama huyu ni ngumu kumuelewa, maana kuna sura moja utaona ni mtu mzuri na hata akifanya ubaya baadaye anabadilika na kurudi kuwa mwema,” alisema Sukambi.

“Mtu ambaye anaishi na mtu wa aina hii anaweza kupata wakati mgumu kuondoka au kujinasua kwenye ukatili akiamini atabadilika. Njia rahisi ya kujiepusha na hawa watu ni kukaa mbali nao, hawa wanapenda kutawala mtu kihisia, kifikra hivyo kuingia kwenye uhusiano nao inakuwa vigumu kutoka.

“Kama umegundua mwenzi wako ana tatizo hili suluhisho ni kuondoka na usirudi nyuma kwa kuwa inaweza kumuongezea hasira na ukatili. Hii kufikiria wanaweza kubadilika, si kweli, kwanza wenyewe hawajui kama wana hilo tatizo na ikitokea umejaribu kumuonyesha utakuwa adui yake. Nisingeshauri kuvumilia linapokuja suala la kupigwa.”

Sukambi alisema ni vyema jamii ikabadili mtazamo na kuwa tayari kuwapokea wanawake ambao wamekimbia ukatili kwenye ndoa zao bila kuwashambulia au kuwakebehi kuwa ndoa zimewashinda na kusababisha familia kuvunjika, bali wawatie moyo na kuwatafutia dawa wanaume wenye tatizo la kupiga wake zao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments