VITA YA MSHAMBULIAJI MAYELE NA MABEKI SIMBA SC BADO NGUMU

 

VITA ya kupata bao mbele ya mabeki wa Simba SC, Mshambuliaji wa Yanga SC Fiston Kalala Mayele imeshindikana msimu huu baada ya Mchezaji huyo kushindwa kuifunga tena Simba SC tangu alipopata bao katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi (Ngao ya Hisani) ambapo Wananchi waliondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mnyama, Septemba 25, 2021 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mshambuliaji Fiston Mayele aliahidi kuwa katika msimu huu amewabakisha na anatamani kuzifunga timu za Simba SC na Namungo FC, tayari kwa Namungo alifanikisha kuwafunga katika ushindi wao wa bao 2-1 kwenye mchezo uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mchezo uliochezwa April 23, 2022.

Kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu uliopigwa Desemba 11, 2021 kwenye dimba hilo hilo la Benjamin Mkapa timu hizo zilitoka sare ya 0-0, huku Mayele akishindwa kutamba mbele ya mabeki wa Simba SC, Henock Inonga Baka na Joash Onyango ambao walifanikiwa kumdhibiti vizuri.

Simba na Yanga SC michezo yote miwili ya msimu wa 2021-2022 imetoa sare ya 0-0, ikiwa wote wamelindiana heshima katika Ligi Soka Tanzania Bara, na huenda wakakutana tena kwenye Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la ASFC msimu huu endapo Simba SC itashinda mchezo wake wa Robo Fainali dhidi ya Pamba FC ya Mwanza, mchezo ambao umewekwa kiporo kutokana na Simba SC kushiriki Michuano ya Kimataifa.

Baada ya matokeo ya sare ya 0-0 katika mchezo wa leo, Yanga SC wanaendelea kubaki kilele kwa alama 55 na michezo 21 huku Simba wakifisha alama 42 na michezo 20 pekee, wakati Yanga SC wakibakisha michezo tisa na Simba SC wakibakisha michezo kumi.

Hata hivyo, vita nyingine ipo kwenye kuwania nafasi ya nne bora ya Ligi hiyo, ambapo nafasi hiyo inawaniwa na timu za Azam FC, Namungo FC, Geita Gold FC, Mbeya City FC sambamba na timu za Kagera Sugar FC na Polisi Tanzania FC.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments