Wabunge Kenya Wanyang’anywa Simu, Kisa Raila

 Wapelelezi wanaofuatilia tukio la kushambuliwa kwa mawe mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga wanashikilia simu za wabunge wawili na Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu, David Kaplagat.

Aprili mosi Raila akiwa amekwenda kuhudhuria maombolezo ya kifo cha rafiki yake, Jackson Kibor, kwenye mji wa Kabenes, jimbo la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu, helikopta aliyokuwa anaitumia ilishambuliwa kwa mawe.

Wabunge ambao imeelezwa kuwa simu zao zinashikiliwa na polisi ni Oscar Sudi wa jimbo la Kapseret na Caleb Kositany ambaye anawakilisha jimbo la Soy, vilevile Spika Kiplagat wa Bunge la Uasin Gishu.

“Wamechukua simu zetu za mkononi na wanazishikilia kwa kile wanachosema ni kuwasaidia katika kufanya upelelezi wa kina. Tulikuja hapa polisi kutoa mwanga zaidi kuhusu shambulizi la Ijumaa na tumejieleza vizuri mbele ya wapelelezi,” alisema Kositany.

Jumapili iliyopita, saa 6:56 mchana, gari nyeusi, Toyota Land Cruiser Prado, likiwa limewabeba wabunge hao wawili liliwasili kwenye Ofisi ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkoa wa Rift Valley, ikiwa ni kuitikia wito wa jeshi.

Jumamosi iliyopita, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkoa wa Rift Valley, Mwenda Boss, aliwaita wanasiasa hao watatu, akiwatuhumu kuandaa na kufadhili shambulizi alilofanyiwa Raila Ijumaa iliyopita.

Mapema Jumapili, Spika Kiplagat alikuwa wa kwanza kuitikia wito makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Rift Valley.

Saa 11:30 jioni, ndipo Kiplagat alitoka, lakini akiwa ameacha simu yake ya mkononi.

Sudi na Kositany, walihojiwa kwa saa 4 mfululizo. Inaelezwa kuwa vijana 14 waliokamatwa wakihusishwa kuwa sehemu ya walioshiriki kumshambulia Raila kwa mawe, waliwataja wanasiasa hao kuwa ndio waliowatuma.

Muda mfupi baada ya kumaliza mahojiano na polisi, Sudi aliviambia vyombo vya habari kuwa Serikali ilianza kutumia vyombo vya dola kuwakandamiza wapinzani wa Raila.

“Kilichotokea leo ni matumizi ya kawaida ya vyombo vya dola ikiwemo Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili kuwakandamiza washirika wa Naibu Rais, William Ruto. Tunashughulikiwa na aina hii ya ukandazaji, lakini ukomo wake ni Agosti 9,” alisema Sudi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu, Raila anachuana na Ruto, ambaye anasimama kugombea kwa tiketi ya Kenya Kwanza. Rais Uhuru Kenyatta, anampigia chapuo Raila ili ashinde urais, ndio maana timu ya Ruto inalaumu kuchezewa rafu na vyombo vya dola.

Kwa mujibu wa mmoja wa wapelelezi waandamizi wa ofisi ya DCI, Mkoa wa Rift Valley, wanasiasa hao watatu waliitwa kueleza kile wanachokifahamu kuhusu shambulizi alilofanyiwa Raila jimbo la Soy.

“Tunashikilia simu zao ambazo zitatusaidia katika kufanya upelelezi wa kina. Wanaweza kuitwa kwa mara nyingine kwa ajili ya kutoa mwanga zaidi kuhusiana na tukio hilo,” mpelelezi huyo aliiambia The Daily Nation la Kenya kwa sharti la jina lake kutowekwa wazi.

Wakili wa wabunge hao, Kipkoech Ngetich, aliviambia vyombo vya habari: “Waliitwa kutoa mwanga katika tukio la mheshimiwa Raila Odinga kushambuliwa na wateja wangu walikwenda wenyewe ili kuwasaidia wapelelezi kuwakamata watu walio nyuma ya mipango ya shambulizi alilofanyiwa Raila.”

Ijumaa iliyopita, saa 11:50 jioni, msafara wa Raila uliwasili ukiwa na helikopta mbili kwa ajili ya kushiriki maombolezo ya kifo cha rafiki yake, Jackson Kibor.

Kipindi ambacho Raila akiwa bado yupo msibani, shambuzi hilo lililotokea. Inaelezwa kuwa vijana zaidi ya 300 walianza kumshambulia Raila kwa mawe, hata alipopanda helikopta, waliendelea kumrushia mawe hadi kusababisha kioo kuvunjika.

Polisi waliokuwa eneo la tukio kwa ajili ya kumlinda Raila, walilazimika kufyatua mabomu ya machozi na hata kurusha risasi hewani ili kumwezesha Waziri Mkuu huyo wa zamani apande helikopta, lakini bado walizidi kumshambulia hadi kuvunja kioo cha mbele cha moja ya ndege za msafara wa Raila.

Tukio hilo, limelaaniwa na wanasiasa wengi akiwemo Ruto, ambaye alimwomba radhi Raila, akisema: “wote waliofanya kitendo cha kumshambuliwa mheshimiwa Raila Odinga watakuwa wamejutia.”

Upande wa Raila, alisema kuwa kwa namna vijana walivyokuwa wakimshambulia, ilimpa picha kuwa lengo lao lilikuwa kumuua.

“Walitaka kuniua nikiwa kwenye helikopta,” alisema Raila, akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Kaunti ya Pokot Jumamosi.

“Sisi hatujapiga mtu yeyote. Wakati wowote kukiwa na fujo sehemu yoyote sisi huwa tunalaani. Jana niliona vioja, tumekwenda kutoa pole kwenye msiba, vijana wakaja kutushambulia kwa mawe.

“Walirusha mawe kama mvua kwenye gari langu. Nikajiuliza hiki ni nini. Nilipoingia kwenye helikopta, nikaona mtu anarusha jiwe kubwa. Sikuwa na mahali pa kukimbilia. Nilistaajabu sana, nikajiuliza haya ni mambo gani? Wale jamaa walitaka kuniua,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments