AFISA Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi wilayani, Ikungi mkoani Singida Yahaya Njiku ametoa onyo kali kwa Wazazi na Walezi wenye tabia ya kuwarubuni watoto wao waache kwenda shuleni huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutaka kuwaoza.
Njiku alitoa onyo hilo jana alipokuwa akizungumza na wazazi na wanafunzi wakati wa ziara yake ya kukagua miradi katika Shule ya Sekondari Munkinya ilioyopo katika kata hiyo.
" Hivi karibuni kumezuka tabia ya baadhi ya wazazi kuwarubuni watoto wao waache shule ili wabaki nyumbani kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuwaoza na wengine wanaambatana na watoto wao mpaka ofisi za Serikali za Vijiji na kata ambako wamekuwa wakitoa madai eti watoto wao hawataki shule hivyo wanaomba wafutwe" alisema Njiku.
Njiku alisema mzazi au mlezi atakaye bainika akifanya hivyo hatamvumilia atamkamata na kumfikisha kwenye vyombo cha dola na katika jambo hilo hata kuwa na huruma na mtu.
Alisema ni jambo la ajabu kwa mzazi na mlezi kufanya jambo hilo kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuboresha miundombinu mashuleni ili watoto wapate elimu katika mazingira bora alafu anatokea mzazi akidai anataka mtoto wake aachishwe shule.
" Itakuwa Serikali ya ajabu ambayo itaukubali upuuzi huo nasema ole wake mzazi tukakaye mbaini akifanya hivyo" alisisitiza Njiku kwa ukali.
Alisema ni wajibu wa wazazi na walezi kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya elimu wawapo shuleni na nyumbani lakini si kwa kuwarubuni kuacha shule.
Njiku alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani kwa kuwapatia kiasi cha Sh. Milion 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili katika shule hiyo ambapo aliwasisitiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii.
0 Comments