Bavicha Yaitaka Serikali Kupunguza Ukali wa Maisha

Siku moja baada ya kupanda bei za mafuta, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Maendeleo (Bavicha), John Pambalu ameitaka serikali kupunguza tozo na kodi ili kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.

Pambalu ametoa kauli hiyo leo Mei 4, 2022 wakati wa Kongamano la madai ya Katiba, lililofanyika Jimbo la Nachingwea, mkoani Lindi, akishangazwa na ukimya wa Serikali kutazama bei za mafuta, bei za bidhaa zikiendelea kuwa juu huku ikikwepa kutoa tangazo la kuimarisha mishahara siku ya Mei Mosi.

Pambalu amesema Serikali ina uwezo wa kupunguza tozo inazokusanya katika mafuta badala ya kujificha katika kivuli cha upandaji wa bei hizo soko la dunia huku ikilinganisha bei za mafuta na mataifa mengine.

Pambalu aliyeanza ziara hiyo Mei Mosi katika majimbo manne kwa lengo la kutoa elimu ya umuhimu wa madai ya katiba mpya, ameitaka serikali kuacha siasa za kulinganisha bei hizo zinazoathiriwa na hali za kipato cha wananchi.

 “Mafuta yanapopanda, nauli zinapanda, bei za vitu zinapanda, kama gharama za usafirishaji wa mchele kutoka Mbeya kuleta Nachingwea ilikuwa ni Sh2milioni, itafika Sh2.5milioni, mnunuzi atalipa ongezeko hilo,”amesema Pambalu anayetarajia kumaliza ziara yake siku tatu zijazo.    

“Rais anaweza asione athari hiyo, waziri anaweza asione athari hizo kwa sababu anawekewa mafuta kwa hiyo Bavicha tunatoa rai rais (Rais Samia Suluhu Hassan) apunguze kodi, tozo na ushuru kwenye mafuta ili gharama zishuke za maisha.”

Siku chache zilizopita, Mawaziri: Dk Mwigulu Nchemba wa Wizara ya Fedha na Mipango na Ashatu Kijaji wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara walitoa mwelekeo wa kunusuru mzigo wa kupanda bei ya bidhaa kwa wananchi huku wakiahidi kupunguza tozo inazochukua katika mafuta.

Hata hivyo hadi sasa serikali haijatangaza mabadiliko yoyote kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), tozo sita (Sh67.01) zinazokusanywa na mamlaka za Serikali ni huduma za bandari (Wharfage) kati ya Sh20.88 hadi Sh22.65, tozo ya ukaguzi wa TBS sh1.24.

Pia kuna tozo ya vipimo chini ya Wakala wa Vipimo (WMA) Sh1 na ada ya kushughulikia masuala ya huduma za forodha Sh4.80, ada ya TASAC sh3.54 na ushuru wa Ewura kati ya Sh6.10 hadi Sh6.80.

Jana, Ewura ilitangaza kuanza kutumika kwa bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo Jumatano Mei 4, 2022 ambapo bei ya nishati hiyo imeendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Jumanne Mei 3, 2022 bei ya mafuta ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam itakuwa Sh3, 148 na dizeli Sh3,264 kwa lita.

Mkoa wa Tanga bei ya petroli itakuwa Sh3, 161 wakati dizeli itakuwa Sh3,264 huku mkoa wa Mtwara peroli ikiuzwa Sh3,177 na dizeli Sh3,309 kwa lita.

Ewura imesema bei ya mafuta ya taa katika Jiji la Dar es Salaam itakuwa ni Sh3112 kwa lita na kwamba mabadiliko ya bei za mafuta nchini yanatokana na kuongezeka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments