Bei petroli, dizeli zaongeza makali kupaa kwa bidhaa



 
Bei mpya ya dizeli na petroli iliyoanza kutumika juzi inatajwa kuwa inaongeza gharama za maisha, hali iliyoibua mawazo tofauti kwa wadau waliotoa namna ya kukabiliana nayo, huku watoa huduma za usafiri wakisema hawawezi kuendelea na nauli za sasa.

 Ikilinganishwa na mwezi uliopita, bei ya petroli kwa Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh287 kutoka Sh2,861 hadi Sh3,148 kwa lita moja, huku dizeli ikipanda kwa Sh566 kutoka Sh2,692 hadi Sh 3,258 katika kipindi hicho.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inasema mabadiliko hayo ya bei yanatokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia inayochangia asilimia 93 na gharama za uagizaji (premium) zinazochangia asilimia nne.

Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema kuongezeka kwa bei ya mafuta kutapandisha kila kitu, hivyo gharama za maisha pia.

“Viwanda vinategemea mafuta kwa sehemu kubwa, usafirishaji hauwezi kufanyika bila mafuta, hata mashambani matrekta yanatumia mafuta. Mzalishaji hana shida sana na kuongezeka kwa gharama hizo za uendeshaji, anachokifanya anazihamishia kwa mlaji,” alisema Dk Pastory.

Hali ya kupanda kwa bei ya mafuta alisema itapandisha bei ya huduma na bidhaa nyingine, hivyo uwezo wa kununua wa walaji utapungua.

Dk Pastory alisema ili kunusuru watu na athari za kupanda kwa bei ya nishati hiyo muhimu, Serikali iangalie namna ya kuweka ruzuku au kupunguza baadhi ya tozo na kodi ili kutoa unafuu, huku waajiri wakiangalia namna ya kuongeza masilahi ya wafanyakazi wao kuwawezesha kumudu gharama za maisha.

Mchumi na mtafiti mwandamizi, Dk Hoseana Lunogelo alisema licha ya kuongezeka kwa bei, bado upatikanaji wa mafuta ni wa uhakika kutokana na kutumia mfumo wa ununuzi wa pamoja (BPS) hivyo kuondoa wasiwasi wa kusimama kwa uzalishaji.

Alisema jambo lililobaki changamoto katika sekta ya mafuta nchini ni gharama za usambazaji baada ya mzigo kufika bandarini kwenda kwa mteja, akisema kutumia malori kunaongeza bei ya nishati hiyo, kwani gharama huwa kubwa hivyo akashauri kuendelea kutanua mtandao wa reli ili mafuta yasafirishwe kwa njia hiyo yenye gharama nafuu.

Dk Lunogelo alisema mfumo wa ununuaji mafuta kwa pamoja una manufaa makubwa kwa walaji wa mwisho (wananchi) kuliko changamoto zake, akisema iwapo BPS isingekuwapo kusingekuwa na uhakika wa usambazaji wa mafuta na bei ingekuwa kubwa zaidi ya inayoshuhudiwa sasa.

“Mambo yangekuwa tofauti kama mafuta yangekuwa yanaingizwa, ingekuwa vigumu hata kuweka bei elekezi kwa kuwa kila mzigo ungekuwa na gharama zake, kwa hiyo kila muagizaji angejipangia bei,” alisema mkurugenzi huyo mstaafu wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Utaratibu huo, alisema unapunguza gharama kwa kuwa anayepewa zabuni ya kuleta mafuta ni yule anayetoa gharama za chini na gharama za meli zinakuwa chini kwa kuwa mzigo unaletwa kwa wingi. Hata hivyo, gharama hizi anazibeba mteja.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi alisema bei ya mafuta iliyoshuhudiwa katika miezi miwili iliyopita haikutokana na athari za vita vya Ukraine, bali kupanda kwa bei ya soko iliyochangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi baada ya kupungua kwa masharti ya kukabiliana na janga la Uviko-19.

“Tanzania kwa kawaida tunatumia mafuta yaliyonunuliwa miezi miwili iliyopita, hivyo tunayotumia sasa ni yale yaliyonunuliwa Machi ambapo bei ya mafuta ilikuwa juu sana wakati vita ndiyo vinashika kasi,” alisema Mmasi.

Hata hivyo, alisema kuna matumaini bei huenda ikapungua au isiongezeke mwezi ujao kwa kuwa mafuta yatakayotumiwa yalinunuliwa Aprili wakati bei zikiwa chini kidogo ikilinganishwa na ilivyokuwa Machi.

Alisema kupanda kwa bei ya mafuta huenda kukapunguza usambazaji wa nishati hiyo kwa kuwa wamiliki wa vituo vya mafuta watatakiwa kuwa na fedha zaidi ili kuendelea kuuza kiwango kilekile, hali ambayo ni ngumu kwa wenye mtaji mdogo.

Awamu hii, bei ya dizeli imepanda zaidi kuliko petroli ambayo huwa juu mara nyingi. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema kila bidhaa ina bei yake sokoni katika siku husika na gharama yake ya kuisafirisha, lakini kuna uwezekano wa dizeli kutumika kama mbadala wa gesi asilia viwandani.

“Kuna uwezekano mkubwa bei ya dizeli imepanda kutokana na uwezekano wake wa kuwa mbadala wa gesi asilia katika uendeshaji wa viwanda. Mafuta hayo yanaweza kutumika baada ya usambazaji wa gesi Ulaya kuathirika,” alisema Mgaya.

Kwa mwenendo ulivyo, alisema kuna uwezekano bei ikapungua katika miezi ijayo kutokana na hali katika soko la dunia, licha ya kuwa gharama za usafirishaji zimeongezeka kipindi hiki.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema kutokana na ongezeko hilo la bei ya mafuta ambayo huchangia sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji, wanatarajia kukutana ili kujadili na kutoka na maazimio.

“Binafsi naamini tutatakiwa kurudi tena mezani kuzungumza na Latra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini) kujadili kuhusu nauli, ila ngoja tusubiri wajumbe ndio watakaoamua,” alisema.

Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, Chama cha ACT-Wazalendo kimependekeza Serikali kuondoa kwa muda baadhi ya tozo kwenye bidhaa hiyo kwa jumla ya angalau Sh500 katika kila lita moja, kwani hali inazidi kuwa mbaya kwa wananchi.

“Tunafahamu kusimamishwa kwa tozo hiyo kutaathiri bajeti ya Serikali, lakini tunapendekeza kusimamisha kwa muda ununuzi wa ndege na Serikali ibane matumizi yake, ikiwamo kwenye safari za nje, semina na warsha na Bunge la bajeti lifupishwe kufidia kuondolewa kwa kodi hizo za Sh500,” inasomeka taarifa ya chama hicho.

Hali baada ya bei mpya

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Mchanga mkoani Geita, John Fred alisema kutokana na ongezeko la bei ya mafuta, wanalazimika kupandisha bei ya tripu kutoka Sh60,000 hadi Sh80,000 wakati madereva bajaji mkoani Mbeya nao wakiwaza kupandisha nauli mpaka Sh1,000 kutoka Sh500 ya sasa.

Madereva teksi mjini Moshi waliliambia gazeti hili kuwa bei hiyo mpya imewaathiri kwa kiasi kikubwa na endapo hali itaendelea hivyo watalazimika kupaki magari yao na kurudi nyumbani kwa kuwa wateja hawawezi kumudu gharama zitakazowalipa kwa safari.

“Mahali ambapo tulikuwa tukienda kwa Sh3,000 tutalazimika kwenda kwa Sh5,000 na tulipokuwa tukienda kwa Sh5,000 itakuwa kati ya Sh7,000 hadi Sh10,000. Sidhani kama wateja wetu watazimudu, watalazimika kutafuta usafiri mbadala kama bajaji au bodaboda,” alisema Emmanuel Ngoda, dereva.

Mwenyekiti wa chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Emmanuel Mollel alisema utalii utaathirika.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments