Bima Ya Afya Kwa Wote Bado Kizungumkuti

Serikali imeendelea kuwa na kigugumizi cha lini itapeleka bungeni Muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote kama ambavyo imekuwa ikiahidi wakati wote.

 Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ameliambia bunge leo Alhamisi Mei 19, 2022 kuwa Serikali ipo katika hatua za ukamilishaji wa muswada wa sheria hiyo.

Dk Mollel alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi ambaye alihoji Serikali ina mpango gani wa kurahisisha huduma ya upatikanaji wa Bima ya Afya kwa wananchi wake.

Swali hilo limekuwa likiulizwa mara nyingi bungeni ambapo majibu ya Wizara yamekuwa ni hayo kwa kila siku bila kueleza hasa lini muswada huo unapelekwa bungeni kufanyiwa kazi.

“Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua ya ukamilishaji wa Muswada wa Sheria wa Bima ya Afya kwa wote ambao utawezesha kurahisisha huduma ya upatikanaji wa Bima za Afya kwa wananchi wote,”amesema Dk Mollel.

Katika maswali ya nyongeza, mbunge wa Viti Maalumu, Stella Ikupa amehoji kuhusu ucheleweshaji wa kadi za bima ya Afya ambao unapelekea wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaama kukosa kadi hizo kwa zaidi ya miezi sita tangu wanapolipia.

Ikupa pia ameomba kujua ni kwa nini Serikali haitoi mwongozo wa bima hata kwa vifurushi kwa wananchi wanaougua magonjwa ya figo ili waweze kusaidiwa kupata matibabu kwa haraka na usahihi.

Naibu Waziri amesema suala la Bima utaratibu unaelekeza kuwa itachukua muda usizidi miezi mitatu tangu mhitaji anapokuwa amelipia gharama zake hivyo suala la kukaa muda mrefu zaidi ya hapo halikubaliki na kwamba litafuatiliwa kuangalia nini kimesababisha.

Kwa wagonjwa wa figo amesema Serikali inaendelea kulitazama jambo hilo na utakapokuja Muswaada wa Bima ya Afya kwa wote litatazamwa kwa mawanda mapana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments