CAG Awakabidhi Takukuru Ripoti za Nondo Wapigaji

 Wakati wadau mbalimbali hapa nchini wakitaka watumishi wa umma wanaohusika na ubadhirifu wawajibishwe, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema baadhi ya taarifa za ripoti za ukaguzi alioufanya zimechukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya kuzifanyia kazi.

 Pia, CAG Kichere ameshauri Sheria ya Manunuzi ya Umma ifanyiwe marekebisho ili kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kusababisha fedha za umma kufujwa.

Kichere alibainisha hayo jana, katika mkutano uliowakutanisha watendaji wa ofisi ya CAG, wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wanahabari wa vyombo vya habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Alisema sheria ya manunuzi ya umma inatoa mwanya wa fedha za umma kufujwa na watendaji wasio waaminifu kupitia ununuzi wa vitu mbalimbali kupitia zabuni wanazozitangaza.

“Unakuta kitu sokoni kinauzwa Sh1,500 lakini watu wamenunua kwa Sh5,000 na unapofuatilia unaona wamekidhi matakwa na wamefuata sheria na taratibu zinazotakiwa...kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria ya ununuzi ili kunusuru fedha za umma,” alisema.

Alisema Kenya wameshafanya mabadiliko ya sheria kama hiyo, akisema ofisi ya CAG inajielekeza katika thamani halisi ya kitu kilichonunuliwa.

Hivi karibuni changamoto kama hiyo imejitokeza katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambapo ripoti za CAG zilibainisha vifaa vilivyonunuliwa kwa bei kubwa tofauti na uhalisia.

Mei 5, 2022 akiwa mkoani Arusha, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB) kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika na ubadhirifu kwenye manunuzi ya vifaa vya afya katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambavyo vilipaswa kununuliwa kwa fedha za Uviko-19.

Alisema MSD walitakiwa kununua kipimo cha sukari ambacho kwa bei ya kawaida ni Sh150 lakini walinunua kwa Sh300, kipimo cha mkojo bei ya kawaida Sh200 kimoja lakini wakanunua kwa zabuni Sh780, walikuwa wananunua kipimo kidogo cha hamolojia ya mwili kinauzwa Sh2,100 wao wakununua kwa bei ya zabuni Sh4,500.

Aprili mwaka huu, Kichere aliwasilisha ripoti ya ukaguzi wa shughuli za Serikali, mifumo ya udhibiti wa ndani na taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha 2020/21, kuanzia Julai 1, 2020 hadi Juni 30, 2021.

Katika ripoti hiyo, CAG alibaini ubadhirifu katika taasisi mbalimbali, ikiwemo uwepo wa madai ya bima ya afya yaliyohusisha wanaume 56 waliodaiwa kupata huduma ya upasuaji wa kujifungua na wengine kujifungua kwa njia ya kawaida, ni miongoni mwa mambo yaliyobainika katika ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, 2021.

Mbali na hayo, katika ripoti hiyo iligundulika kuwa mashine 89 za makusanyo ya faini za makosa ya usalama barabarani zinazotumiwa na trafiki hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo wa malipo wa Serikali.

Katika mkutano wake wa jana, Kichere alipata fursa ya kutoa mada na kujibu maswali ya wahariri ambapo baadhi ya wahariri, wakiwemo Joseph Kulangwa na Salim Said Salim walimuuliza Kichere anajisikiaje mapendekezo ya ripoti zake kutofanyiwa kazi

Katika majibu yake, Kichere alisema kila mkaguzi anapenda kuona ripoti, maoni na mapendekezo anayoyatoa yanafanyiwa kazi ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza zisijirudie katika kaguzi zijazo.

Kichere pia alisema tatizo jingine ambalo analiona ni baadhi ya fedha za Serikali kutumiwa bila kupita katika mfuko mkuu (hazina) ambao yeye ndiyo anaidhinisha.

“Hili jambo lilionekana sana, inaonekana fedha nyingi ni zile za miradi zinazotoka kwa wafadhili na kwenda moja kwa moja kwenye miradi husika,” alisema.

Kuhusu gawio

Kichere alisema baadhi ya mashirika ya umma yalitoa gawi kwa Serikali, lakini kwake fedha walizotoa walisema ni mchango.

“Gawio haliwezi kutolewa na shirika linalopata hasara, hivyo wale waliosema wametoa gawio ama walikosea au walifanya hivyo kwa makusudi,” alisema.

Katika mkutano huo, Kichere alisema vyombo vya habari ni wadau muhimu na vina mchango mkubwa katika kuimarisha utawala bora na kuchagiza mahitaji ya uwazi katika shughuli za Serikali kwa kuelimisha jamii kwenye masuala yenye tija kwa Taifa.

Alivishukuru vyombo vya habari namna vinavyotekeleza majukumu yake kufikisha taarifa za ripoti za ukaguzi unaofanywa na ofisi yake. Alisema ameshuhudia namna ambavyo vyombo vya habari vinatoa ufafanuzi wa ripoti za CAG baada ya kuwasilishwa Bungeni.

“Taarifa zenu huwa tunazotumia kupata maeneo hatarishi katika suala la usimamizi wa rasilimali za umma kisha kuandaa mpangokazi na ukaguzi katika eneo hilo,” alisema Kichere.

Akizungumza na kwa niaba TEF, Salim Said Salim alisema Ofisi ya CAG imefanya jambo jema kuandaa mkutano huo uliowaongezea uelewa wahariri na waandishi hivyo akataka ushirikiako huo uboreshwe zaidi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments