CCM MANYARA WAKABIDHI KADI BIMA YA AFYA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM MAGUGU

Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Manyara umekabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto wenye uhitaji maalum 50 wanaosoma katika Shule ya Msingi Magugu mkoani hapa.


Kadi hizo za bima ya afya kwa watoto hao zimekabidhiwa jana Mei 14,2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Manyara ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Taifa Shaka Hamdu Shaka.

Shaka alikabidhi kadi hizo baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara Naomi Kapambala kumuomba akabidhi kadi hizo ambazo zimetokana na fedha za michango ya wanawake wa Chama hicho mkoa ambao waliamua kuchangishana ili kusaidia wanafunzi hao wenye uhitaji.

Akielezea zaidi kabla ya kukabidhiwa kwa kadi hizo Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Manyara amefafanua wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Duniani walitembelea Shule ya msingi Magugu na miongoni mwa maombi yaliyotolewa na walimu wa shule hiyo ilikuwa ni kadi za bima ya afya.

“Tukiwa pale pamoja na mambo mengine moja ya jambo ambalo walisema wanalihitaji sana ni bima ya afya ili kuwasaidia katika kupata huduma za afya.Hivyo leo tunao baadhi ya walimu na wanafunzi kwa ajili ya kukabidhi kadi za bima ya afya ambazo tunaomba Mlezi wetu ukabidhi kwa niaba yetu,”amesema Kapambala.

Kwa upande wa walimu wa shule hiyo, wamesema kwamba katika shule hiyo kuna wanafunzi 56 wenye uhitaji maalum na kupatiwa kadi za bima ya afya na chama hicho ni jambo la kushukuru na kupongeza.

“Tunao watoto wenye mtindio wa akili na usonji na tunawalea katika makundi tofauti kuna kundi la kwanza ambalo lenyewe tunalifundisha majumbani kwao na kundi la pili lile lenye watoto wenye unafuu na kundi la tatu ni watoto ambao hao wananafuu kubwa na hivyo wanasoma madarasani.

“Kupata kadi hizi 50 kwetu ni jambo la faraja.Nitoe rai kwa wale wenye kujiweza waendelee kusaidia watoto wetu kwani wana changamoto nyingi ambazo zinahitaji msaaada wa kila mmoja wetu,’amesema mmoja ya walimu wa shule hiyo mbele ya Shaka.

Kwa upande wake Shaka amesema amepata nafasi ya kusikiliza changamoto ambazo zinawakabili wanafunzi hao , hivyo ameamua kuchangia sh.500,000 kwa ajili ya kusaidia kutatua baadhi ya changamoto, huku akiomba wengine wenye uwezo kuchangia.

 

Katibu  wa Itikadi na Uenezi  CCM Taifa  Shaka Hamdu Shaka, akiwa amembeba Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Magugu kitengo cha Watoto Wenye Mahitaji Maalum Azmina Swedy mara baada ya kumkabidhi kadi ya Bima ya Afya iliyotolewa msaada na Uongozi wa CCM Mkoa wa Manyara.
Katibu  wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa  Shaka Hamdu Shaka, Akipewa Rungu na Laiguanani Mkuu wa Jamii ya Watu wa Simanjiro ikiwa ni Ishara ya Kumsimika kuwa kiongozi wa Ngazi ya Juu katika jamii hiyo na Kumpa Jina La “OLE SHAKA”
 Na Said Mwishehe.Manyara

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments