Chammata, Serikali kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini

 Chama cha Wafanyabiashara wa Kati wa madini nchini (Chammata), kimejipanga kushirikiana na Serikali kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 20, 2022 jijini Arusha na Mwenyekiti wa Chammata Taifa, Jeremiah Kipuyo katika mkutano wa uzinduzi wa katiba na kanuni za chama hicho chenye wajumbe kutoka mikoa yote ya kimadini nchini.

Amesema suala la utoroshwaji lazima likomeshwe hivyo watashirikiana na serikali ili wanaojihusisha na vitendo hivyo wachukuliwa hatua za kisheria.

"Tunahakikishia serikali baada ya muda mfupi suala la utoroshwaji madini litakuwa historia, sisi tutaungana na serikali kuhakikisha utoroshwaji unapotea.

"Tutashirikiana kudhibiti madini feki yasiingie sokoni kwani siku za nyuma tulisikia huko Ulanga madini feki yamekamatwa kwenye hili tutapambana na wanaoingiza madini feki sokoni kwani linaumiza wafanyabiashara na hawatakaa salama wataenda kwenye mikono ya sheria," amesema.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema wizara hiyo inatarajia hadi Juni 2023 kukusanya Sh822 bilioni ikiwa ni makusanyo ya kodi ya wafanyabiashara wakubwa wa kati na wadogo wa madini.

Amesema kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha sekta hiyo inaongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

"Mwaka 2016, ilikusanywa Sh213 bilioni, mwaka 2017 Sh301 bilioni, mwaka 2021 Sh584.8 bilioni na mwaka 2022/23 tunarajia kukusanya Sh822 bilioni hadi Juni mwakani,” amesema.

Dk Kiruswa amesema mchango wa wafanyabiashara katika makusanyo ya serikali umekuwa  ukiongezeka kila mwaka kutokana na ushirikiano kati ya  uongozi wa Femata na Tamida na uwepo wa masoko na kupungua kwa utoroshaji wa madini.

Amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 6.7 mwaka 2020.

 

Post a Comment

0 Comments