Huyu ndiye Martha Karua wa Raila Odinga

Kitendawili cha muda mrefu kuhusu jina la mgombea mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya kimeteguliwa. Jina lililopenya ni la Martha Karua.

Sasa, mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, atasimama bega kwa bega na Martha, kuomba ridhaa ya Wakenya ili wawachague kuliongoza taifa hilo kati ya mwaka 2022 na 2027.

Raila akimtangaza Martha, alimwelezea kuwa ni mwanamke mpiganaji, asiyekimbia mapambano, hivyo atakuwa Naibu Rais bora kwa Kenya.

Awali, kabla hajataja jina la Martha, alieleza kuwa Kenya inaelekea kutimiza miaka 60, na katika kipindi chote hicho, taifa hilo halijawahi kuwa na Rais, Naibu Rais au Makamu wa Rais mwanamke.

“Nahitaji Joshua wa kweli kwenye uongozi wangu, mtu ambaye hatakuwa msaliti. Baada ya kutafuta kwa muda mrefu, kuakisi na ushauri mbalimbali, nimefikia kwenye uamuzi kuwa mtu anayetakiwa kushika nafasi ya mgombea mwenza wangu lazima awe mwanamke,” alisema Raila katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC).

Raila aliongeza: “Ofisi ya Naibu Rais haiwezi kushindana na ya Rais. Mtu anayetakiwa kuwa Naibu Rais anapaswa kuwa mfanyakazi mwenza na sio hasimu.”

Raila anaposema anahitaji Joshua wa kweli, anakuwa anafanya marejeo kwenye Biblia kuhusu Musa na mwanafunzi wake, Joshua. Kisha Joshua akawa msaidizi mwaminifu wa Musa. Wakafanya kazi kwa imani na utii wa hali ya juu katika kuwatoa wana wa Israel Misri mpaka Canaan, nchi ya Ahadi.


Uamuzi wa Kalonzo

Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka alifanya kampeni na kushinikiza yeye ndiye ateuliwe kuwa mgombea mwenza, nafasi ambayo imekwenda kwa Martha.

Mchakato wa kupata jina la mgombea mwenza ulichakatwa na kamati maalumu iliyoundwa na Baraza la Azimio linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Raila alisema baada ya kupitia ripoti ya kamati, anamteua Kalonzo kuwa Waziri kiongozi wa serikali yake baada ya Azimio la Umoja kushinda uchaguzi.

“Pia namteua Kenneth Marende kuwa spika wa seneti. Vilevile namteua Wycliffe Oparanya kuwa Waziri wa Fedha,” alisema Raila.

Akiendelea kugawa nafasi, Raila alimtaja Peter Munya kwamba atakuwa Waziri wa Kilimo, Gavana wa Mombasa, Hassan Joho alimpangia uwaziri wa Ardhi.

Hata hivyo, Kalonzo hajaridhika. Tayari ameshatangaza kujiweka kando na muungano huo.

Wakati Raila akiendesha mkutano na waandishi wa habari KICC, Kalonzo naye alikutana na wanahabari kivyake. Katika mkutano wake, Kalonzo alimtakia Martha kila la heri kwa uteuzi aliopewa.

“Namwombea mema mgombea mwenza wa Raila, Martha Karua. Tumekubaliana tugawanyike. Nilimwambia Raila kuwa uamuzi wa kumfanya Martha Karua kuwa mgombea mwenza utakutana na upinzani mkubwa.

OKA (One Kenya Alliance), tutasimama peke yetu na muda si mrefu tutazindua ilani yetu,” alisema Kalonzo.

Martha, alijiunga na Azmio la Umoja Machi mwaka huu na tangu alipojiunga amekuwa akizunguka nchi nzima ya Kenya akimfanyia kampeni Raila.

Wiki iliyopita, Martha alihudhuria usaili ulioendeshwa na kamati ya uteuzi wa jina la mgombea mwenza. Baada ya kutoka kwenye usaili Martha alisema angeridhika na uamuzi wowote wa kamati.

“Nilikwenda kwenye usaili bila orodha ya masharti. Nilikwenda nikijua hali halisi na nitaendelea kufanya nao kazi hata kama yatakuja matokeo yoyote,” alisema Martha baada ya usaili.

Msisitizo wa Martha ulijikita kwenye kutambua ubora wa Raila, akifafanua kwamba katika watu wote waliojitokeza kuwania urais mwaka huu, hakuna anayekaribia sifa alizonazo Waziri Mkuu wa Kenya aliyehudumia nchi kati ya mwaka 2008 mpaka 2013.

“Historia yangu na ya Raila zinafanana. Raila ni mzalendo ambaye ambaye amepigania haki za binadamu maisha yake yote. Nipo Azimio kwa sababu namfahamu Raila anabeba masilahi ya umma ndani kabisa ya moyo wake.

Hata pale anapokosewa hufanya uamuzi kwa kutazama masilahi ya watu,” alisema Martha.

Akieleza zaidi sababu za yeye kusimama na Raila, Martha alisema rekodi za kiongozi huyo wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kusimama na Wakenya zipo wazi, kwa hiyo ndiye mtu bora zaidi kuwa Rais.

“Tunapozingatia matukio kama ya mwaka 2002, 2007 na 2013, tutakubali kuwa Raila huweka masilahi yake pembeni kwa ajili ya Wakenya. Ni aina gani ya kiongozi tunayemtaka kama si yule ambaye anayeweka mbele masilahi ya Wakenya. Hakuna upande mwingine wana kiongozi wa aina hiyo,” alisisitiza Martha.

Kikubwa ambacho Martha amekuwa akisisitiza ni kwamba Wakenya wanachotakiwa kuzingatia mwaka huu si kutazama vyama, bali mtu ambaye anaweza kuifaa Kenya na watu wake.

“Hebu tupimeni watu hawa watu wote wanaoutaka urais, tuone ni wa aina gani. Kuna wazuri na wabaya kila upande, lakini hakuna hata mmoja anayekaribia vigezo vya Raila,” alisema Martha.

Uteuzi wa Karua kuwa mgombea mwenza umekuja siku moja baada ya Naibu Rais, William Ruto anayegombea urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza kumteua Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments