IFAD: Ukame Na Vita Vya Ukraine Vimewaathiri Pakubwa Wakulima Nchini Somalia

Mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo (IFAD) umetahadharisha kwamba ukame na vita vinavyoendelea nchini Ukraine vimesababisha athari kubwa kwa wakulima nchini Somalia.
Taarifa ya asasi hiyo inaeleza kuwa, kutokana na athari hizo hivi sasa wakulima nchini Somalia wanahitaji msaada wa haraka ili kunusuru kilimo na maisha yao kabla hali haijageuka na kuwa janga kubwa la kibinadamu.

Mmoja wa wakulima hao anasema: Kama wakulima tumeathirika vibaya na ukame, visima tulivyokuwa tukitumia kumwagilia mashamba yetu sasa vyote vimekauka na mashamba yetu yako hatarini kuvamiwa na wanyamapori. Wao pia wameathiriwa na ukame na wanakuja kusaka malisho, pia tumepoteza mazao mengi tuliyotarajia kuyavuna.”

Kwa mujibu wa IFAD ukame huu nchini Somalia umesababisha njaa na ugumu wa maisha kwa wakulima, na miezi miwli iliyopita hali imekuwa mbaya zaidi, kwani vita vinavyoendelea nchini Ukraine vimechochea kupanda kwa bei ya mafuta na mbolea kwa asilimia 40, na majanga hayo mawili ukame na vita yamefanya wakulima kupata hasara kubwa.
                                                                                              

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutolewa misaada ya haraka ya kuweza kuwaokoa wananchi wa Somalia kutokana na ukame kuhatarisha vibaya maisha ya asilimia 40 ya wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika taarifa yao ya jana Jumanne, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO pamoja na mashirika ya OCHA, UNICEF na WFP ambayo yote yanafanya kazi chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa, yamesema kuwa, watu milioni sita wanakabiliwa na kiwango kidogo mno cha chakula nchini Somalia na misaada ya haraka mno inahitajika ili kuokoa maisha yao.

Post a Comment

0 Comments