Kashfa sare Za Wafanyakazi Mei Mosi Moto

Sare za wanachama cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu) kwa ajili ya kuvaa kwenye sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) zimezua malumbano baada ya kubainika kuwa chini ya kiwango.

Talgwu ndiyo iliyoratibu sherehe hizo kitaifa chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), zilizofanyika jijini Dodoma jana, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.

Wakati Mwenyekiti wa Talgwu ambaye pia ni Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya akimnyooshea kidole mzabuni aliyepewa kazi ya kuzalisha fulana na kofia hizo (jina linahifadhiwa) kwa ajili ya wanachama, taarifa zilizoifikia Mwananchi zimedai kuwepo kwa harufu ya upigaji wa fedha za chama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Talgwu ilitoa zabuni kwa ajili ya kuchapishwa fulana na kofia 90,000 na kuzisambaza kwa wanachama nchi nzima.

Nyamhokya jana alidai chama chake kupokea fulana mbovu. “Sisi ndio wenye Talgwu na ndio tuliofanyiwa uhuni na huyo mzabuni, kwa hiyo tunazo hizo taarifa.”

Alipoulizwa sababu ya kumpa kazi mzabuni anayefanya kazi chini ya kiwango, Nyamhokya alidai kuwa walifuata vigezo vyote.

“Sisi tumempa mzabuni na ndiye mwenye kazi, sasa alikwenda kuchapishia wapi, huo ni wajibu wake yeye. Of course chama kina mechanism zake, kuna bodi ya zabuni na inatolewa kwa mtu mhusika na taratibu zote za zabuni. Kwa hiyo makosa yakifanywa na mzabuni, zipo taratibu za kufuatwa, ikiwa pamoja na kumbana ili afidie hizo hasara.

“Huyo mtu anafanya zabuni za serikali na alivyokuja huku na CV zake zikaonekana, kwa hiyo tender board yangu wakam award,” alidai Nyamhokya.

Huku akimtaka mwandishi kumtafuta Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Mtima, Nyamhokya aliendelea kusema kuwa, baada ya kuona fulana hizo hazifai, wamesitisha ugawaji kwa wanachama.

“Baada ya kugundua tumesitisha kugawa, tunajaribu kuangalia namna nyingine ya kufanya watu wetu wanaoandamana kuvaa T-Shirt. Kwa hiyo zile taratibu nyingine zinaendelea baada ya kumaliza Mei Mosi hizo zitafuata,” alisema.

Hata hivyo, Mtima hakupatikana kueleza undani wa sakata hilo wakati wote alipopigiwa simu na ujumbe aliotumiwa hakuujibu.

Mwananchi limeona barua kutoka makao makuu ya Talgwu ya Aprili 28, 2022 kwenda kwa makatibu wa mikoa Tanzania Bara ikiwaomba radhi kwa sare hizo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments