Kilichomkuta Katambi Chamtokea Kasekenya Bungeni

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa mara nyingine tena leo amemtaka Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya kurudia majibu katika swali la mbunge wa Handeni Mjini, Reiben Kwagilwa kwani majibu yake ya awali hayakuwa sahihi.

 Leo Jumatatu Mei 23, 2022 ni mara ya tatu Spika Dk Tulia kutoa maagizo ya kurudiwa kujibiwa maswali ya wabunge katika mkutano huu wa saba wa bunge la 12 unaoendelea jijini Dodoma kwa madai yanajibiwa na Naibu Mawaziri bila ukamilifu.

Wiki iliyopita, Dk Tulia aliamuru Naibu Mawaziri Patrobas Katambi na Omar Kipanga kutoa majibu ya kina kwa wabaunge kutokana na majibu waliyokuwa wameyatoa kulalamikiwa kuwa hayakuwa na uhakika na baada ya Spika kupitia kumbukumbu rasmi alikiri kuwa naibu mawaziri hawakuwa na majibu ya kujitosheleza.

Leo Kasekenya ameagizwa kurudia majibu ya swali la Kwagila kuhusu ujenzi wa barabara ya Handeni-Mafuleta yenye umbali wa kilomita 20 ambalo alilijibu mwishoni mwa wiki.

Kwenye majibu hayo, Naibu Waziri alieleza kuwa taratibu za ujenzi wa barabara hiyo zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba ili kazi ianze.

Hata hivyo alipoulizwa swali la nyongeza alisema kuwa mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo yuko eneo la ujenzi kwa ajili ya kazi majibu ambayo yalionekana kutofautiana hivyo muuliza swali akaomba mwongozo wa Spika.

“Baada ya kujiridhisha nimebaini kuwa, ni kweli swali la mbunge halikujibiwa kikamilifu kama ilivyotakiwa, na kwa mujibu wa kanuni yetu namba 53 inayoelekeza swali kupatiwa majibu kikamilifu, naagiza swali hilo lijibiwe upya,” amesema Dk Tulia.

Spika amewaagiza wabunge wanapouliza maswali ya nyongeza yaendane na maswali ya msingi ili waweze kupata majibu ya uhakika na kuwataka mawaziri na naibu mawaziri kuacha kujibu maswali ya wabunge kwa mzaha.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments