Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo wajumbe wa Chadema walikwenda mkoani Dodoma juzi na kikao hicho kilianza jana mchana.
Mwananchi limedokezwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyotawala kwenye kikao hicho ni mchakato wa Katiba mpya, maridhiano ya kisiasa, tume huru ya uchaguzi na suala la wabunge 19 waliovuliwa uanachama na Chadema, lakini wanaendelea na ubunge wao baada ya kufungua kesi ya kupinga kufukuzwa kwao.
Jitihada za Mwananchi, kupata undani wa mazungumzo hayo hazikuzaa matunda, baada ya pande zote mbili kutokuwa tayari kuweka wazi walichojadiliana.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo waliozungumza na gazeti hili, walisema ni mapema kuweka wazi walichozungumza na kutaka wapewe muda .
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar) Salum Mwalimu alisema kuwa Mbowe ndiye msemaji wa jambo hilo hivyo kumtaka mwandishi awasiliane naye. Hata hivyo, simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
“Mimi sikwenda kwenye huo mkutano kwa kuwa niko safarini lakini hata ningekwenda kiutaratibu mzungumzaji ni mwenyekiti au katibu mkuu hivyo mkiwatafuta wanaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia” alisema
Mwananchi pia liliwasiliana na Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ambaye pia hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
“Kwa sasa ni mapema kueleza nini kilichozungumzwa, tuvute subira.
Hali ilivyokuwa
Picha za wajumbe wa kikao hicho zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana usiku, huku zikiwaonyesha baadhi ya wajumbe maarufu kutoka vyama hivyo.
Upande wa CCM alikuwapo Rais Samia, Makamu Mwenyekiti (Bara), Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu Daniel Chongolo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.
Kwa Chadema, miongoni mwa watu walionekana kwenye picha hizo ni wakili maarufu Jeremiah Mtobesya ambaye alikuwa akimtetea Mbowe na wenzake watatu waliokuwa wakishtakiwa kwa ugaidi na uhujumu uchumi.
Mwingine ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Catherine Ruge, Mjumbe wa Kamati Kuu, John Heche, Katibu Mkuu John Mnyika, Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Mohamed Issa, wakili Jonathan Mndeme, Reginald Munisi
Pia kulikuwa na baadhi ya viongozi wa Serikali waliohudhuria mkutano huo, wakiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi
Mbowe alivyofichua mkutano
Suala la Chadema kukutana na CCM lilitangazwa na Mbowe katika kikao cha Baraza Kuu kilichoketi Mei 11 jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kila upande utakuwa na wajumbe 10.
Juzi, Mbowe aliongoza ujumbe wa Chadema kuelekea jijini Dodoma na jana walikutana na wajumbe wa CCM wakiongozwa na Rais Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Kukutana kwa vyama hivyo kunakuja wakati tayari Mbowe akiwa ameshakutana na Rais Samia mara mbili Ikulu ya Dar es Salaam.
Mara ya kwanza Mbowe alikutana na Rais Samia alipotoka gerezani, baada ya kesi ya makosa ya ugaidi na uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili pamoja na wenzake watatu, kufutwa Machi 4, 2022.
Akitoa taarifa ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi Machi 16, alisema katika kikao hicho na Rais Samia walijadili njia bora ya kutafuta amani na suluhisho katika kufanya siasa.
“Tulikubaliana aache kuzungumzia neno amani azungumze neno haki. Jambo la tatu nilimfahamisha Chadema ni chama kikuu cha upinzani huwezi kukiacha nje,”alisema Mbowe.
Mkutano huo ulifuatiwa na mwingine wa Mei 9, ambapo Mbowe aliliambia Baraza Kuu mambo waliyojadili ikiwa pamoja na kutafuta njia za kufanya siasa za ushindani.
Alisema baada ya kutoka gerezani alilazimika kukutana na Rais kwa shabaha ya kusimamia masilahi ya Taifa, kutokana na nafasi yake na kupata suluhu ya kinachowatenganisha wapinzani na chama tawala.
Mengine aliyosema kuwa walizungumza ni uwepo wa matabaka miongoni mwa Watanzania na mahubiri ya amani pasi na kujenga msingi wake.
“Tulikubaliana kwamba lazima tujenge kuaminiana katika ngazi zote za uongozi wa nchi yetu, nimechoka kuona viongozi wa upinzani wanapelekwa magerezani, wala sio sifa kuona vijana wa Chadema wanapigwa risasi, “alisema.
Mbowe alisema walizungumza kuhusu haki na amani kwa wapinzani kufanya siasa na kusisitiza kuwa kauli zake hizo zisiwafanye wanachama wa Chadema kurudi nyuma pale wanapoonewa.
“Sisi milango yetu ipo wazi, yeyote anayeamini katika haki kwa nchi yetu, anayeamini ushirika wetu utasaidia tutakuwa tayari kufanya naye kazi wakati wowote,” alisema
0 Comments