Magari mawili yaliyokuwa yanasafirisha bidhaa za magendo kutoka Tunduma kuelekea Mbeya yamekamatwa katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe yakiwa yametelekezwa, baada ya moja aina ya Bravis kupinduka.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoani Sonwe, Dickson Qamara amesema magari hayo ambayo yalikuwa yameongozana katika barabara ya Tunduma-Mbeya moja aina Toyota Crawn liligonga kizuizi kilichowekwa na kikosi kazi cha kuzuia magendo katika eneo la Oldvwawa na kisha kupasuka tairi na kutelekezwa na dereva aliyekuwa akiliendesha.
Hatua hiyo ilitoa nafasi kwa gari lingine aina ya Toyota Brevis kupita ambalo dereva alipobaini kufuatiliwa alichepuka njia na kuzima taa kisha kupinduka baada ya kupanda moja ya tuta lililowekwa barabarani katika eneo la Ichenjezya kwa Jimmy mjini Vwawa wilayani Mbozi na kisha kupinduka na dereva wake pia kutoweka kusikojulikana.
"Gari hili lilikimbia kizuizi chetu tulichokiweka Oldvwawa na kukigonga ndipo lilipopasua matairi yake mawili na katika kututoroka alikimbilia njia ya Ichenjezya na ndiko alipopata hii ajali na pia kuna gari tumelikamata aina ya Crown ambalo lilikuwa likiisindikiza gari iliopata ajali na lenyewe tumelikamata na vitenge na vipodozi" amesema Qamara
Qamara aliwataka wananchi kuacha kujihusiha na vitendo vya kusafirisha au kuuza na hata kununua bidhaa za magendo bali wafuate taratibu za ulipaji kodi na kuacha kuikosesha Serikali mapato.
Shuhuda mmoja Abdala Nzunda amedai kuwa biashara ya magendo katika barabara ya Mbeya-Tunduma imeshamiri kutokana na bidhaa kuuzwa bei nafuu kwa nchi jirani ya Zambia ukilinganisha na hapa nchini.
Hivi Karibuni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba aliunda kikosi maalumu ndani ya Mkoa huo kitakachoshughulikia uzuiaji na ukamataji wa bidhaa za magendo ambapo mpaka mwanzoni mwa mwezi kilifanikiwa kukamata magari kadhaa likiwamo moja la ofisi yake.
Na Stephano Simbeye
0 Comments