Majaliwa aagiza uhakiki vibao vya mitaa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza makatibu tawala wa mikoa kuhakiki vibao vya majina ya mitaa katika anwani za makazi ili kuepuka makosa ya maandishi.

Majaliwa ameyasema leo Ijumaa Mei 6, 2022 wakati akizindua mradi wa Afya yangu unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID).

Amesema kazi ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi inaendelea nchini ambayo inaenda sambamba na anwani za makazi.

Majaliwa amewataka Watanzania kushiriki katika sensa ya watu na makazi na kwamba haitakuwa faida kwa Watanzania tu pekee bali na taasisi zote zinazofanya kazi na Serikali ya Tanzania.

Amesema kazi hiyo inaendelea na imefikia asilimia 86 katika kuikamilisha uwekaji wa anwani za makazi na kwamba kazi iliyobaki ni kuchomeka vibao kuonyesha mitaa.

“Ingawa vibao vingine vimeandikwa kimakosa lakini najua yatarekebishwa. Juzi nilikuwa natembea nikaona bango moja limeandikwa Mahakama load badala ya Road (barabara) imeandikwa load,”amesema.

Majaliwa amewataka makatibu tawala kuangalia usahihi wa majina ya mitaa hiyo.

 “Wanapoandika majina haya mhakiki mara mbili mbili. Msikubali kwenda kubandika kibao kikiwa kimekosewa. Yapo majina ya watu yahakikiwe vizuri,”amesema.

Amesema kuna bango moja limeandikwa kimakosa Feed Force badala ya Field Force na lingine lilikuwa likiandikwa jina lake lakini limekosewa pia.

Kuhusu mradi huo wa USAID Afya Yangu, Majaliwa amewataka watakaoutekeleza kuusimamia vyema mradi huo ambao utatekelezwa katika mikoa 21 nchini ikiwemo Zanzibar ili kuokoa maisha ya watu wengi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema USAID imekuwa ikisaidiana na sekta ya afya katika kuimarisha huduma za afya ya uzazi kwa vijana.

Amezitaja huduma hizo ni pamoja na kujikinga na mimba za utotoni, kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa vijana na kuwapa stadi za kupambana na ukatili wa kijinsia.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini, V kate Somvongsiri amesema mpango huo wa USAID Afya Yangu utagharimu Dola za Marekani milioni 260.

Amesema mradi huo ni wa miaka mitano na utajumuisha mitatu itakayoshughulika na masuala ya VVU, Kifua Kikuu, uzazi wa mpango, afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments