Mbunge aeleza faida kudahili wanafunzi wengi wa nje ya nchi


Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya amesema mwongozo wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), unaohusu udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka nje ya nchi umefanya vyuo vikuu kushindwa kupata wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi.

Dk Chaya ameyasema hayo leo Jumatano Mei 11, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2022/2023.

Amesema bado kuna tatizo kubwa la wanafunzi wanaotaka kuja kusoma nchini jambo ambalo linatokana na mwongozo uliotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Amesema ili TCU imeweka kiwango cha juu cha vyuo vikuu kuchukua wanafunzi kutoka nje ya nchi kuwa ni asilimia tano, jambo ambalo linasababisha vyuo vya nchini kushindwa kushika nafasi za juu katika ubora wa kimataifa.

“Kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaokuja kutoka nje ya nchi kunaongeza ubora na utambuzi wetu kimataifa,”amesema.

Amesema sasa hivi udahili wa wanafunzi kutoka nje ya nchi katika vyuo vya nchini ni ni chini ya asimilia moja tu.

Pia amesema kudahili wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi kutawezesha utalii wa kielimu kufanyika nchini na kwamba wanafunzi hao hawataishia kukaa vyuoni pekee bali watataka kutembelea mbuga za wanyama.

Aidha, amesema Chuo Kikuu Huria (OUT) ndicho pekee kimepewa fursa ya kuwa na foundation course kwa mwanafunzi aliyepata GPA ya chini ya 3.0 anayetoka kusoma shahada.

Amesema hivyo imeleta changamoto kwa wanafunzi waliopata ufaulu mdogo kwenda kusoma shahada kwa fani walizonazo kwasababu kuna kozi nyingine hazipo OUT.

Dk Chaya ameshauri Serikali itolewe katika vyuo vikuu vyote kwasababu OUT imeshalemewa na wanafunzi wengi.

Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mussa Sima akichangia makadirio ya mapato na matumizi hayo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ameshauri Serikali kufanya tathimini kama sababu za kupeleka masuala ya elimu kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kama bado zipo na zina tija.

Sima amesema “Sababu ambazo zilitufanya kuhama kushughulikia walimu na elimu kwa ujumla inawezekana hazipo hivi sasa. Serikali irudi tena ikatazame jambo hili kama bado lina tija kuwaachia Tamisemi kusimamia masuala ya elimu,”amesema.

Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mussa Sima wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2022/2023 leo Jumatano Mei 11,2022. Picha na Merciful Munuo

 Amesema wathibiti ubora wa elimu wameachwa bila kuwezeshwa na matokeo yake hawafanyi kazi kama vile ilivyotakiwa kufanyika.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapaswa kuiwekeza zaidi katika hawa wadhibiti ubora, hawa walikuwa wanapaswa kuwaambia kilichofanyika huku chini lakini hawa,”amesema.

Ameshauri Serikali iwawezeshe wathibiti ubora kufanya kazi yao.

Aidha, amesema ubora wa hauji kama ajali bali matokeo ya fikra nzuri na kuwapongeza   Serikali kuandaa vitabu vya umahiri.

Sima amesema shida katika kutumia vitabu hivyo ni walimu hawajaandaliwa katika ujuzi.

Amesema kama unadaa vitabu vinavyozungumzia ujuzi lakini elimu unayokwenda kuitoa ni ya maarifa, kamwe usitarajie kutakuwa na elimu bora.

Ameshauri Serikali katika bajeti 2022/2023 kutowekeza katika miundombinu bali kujifunza na kufundisha ili kuwapa walimu ujuzi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments