Msimamo Wa Rais Samia Wawaibua Wadau Wa Habari

Wadau mbalimbali wa Sekta ya Habari, Mabalozi na waandishi wa habari wakimsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akitoa hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika Jijini Arusha


Wadau wa tasnia ya habari wamesema wameanza kuona utashi wa Serikali katika kuviacha vyombo vya habari vitekeleze majukumu yake kwa uhuru.

Juzi akiwa jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari barani Afrika, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru, huku wakitanguliza uzalendo na kuielezea vizuri Tanzania.

Rais Samia alimuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kushughulikia maombi ya uwezekano wa kuondolewa au kupunguzwa kodi na ushuru wa forodha na ongezeko la thamani kwa karatasi za kuchapisha magazeti, ikiwa ni mojawapo ya maombi yaliyotolewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Akizungumza na Mwananchi, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Olengurumwa alisema ni wazi kauli ya Rais imeonyesha utashi wa Serikali katika kuviacha vyombo vya habari viwe huru na hilo limeanza kuingia tangu aingie madarakani.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wadau mbalimbali wa Sekta ya habari katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliofanyika Jijini Arusha Mei 3, 2022.


Alisema nia ya dhati ya Rais inapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa kauli zake ambao unapaswa kufanyiwa kazi na watu wanaomzunguka ili kuhakikisha kinachofanyika sasa kinabaki kuwa hivyo siku zote.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tanzania (Misa Tan), Salome Kitomari alisema: “Utashi wa kisiasa upo, kitendo cha Serikali kusikiliza maoni ya wadau na kuwa tayari kukaa nao kufanya marekebisho ya sheria kandamizi kinaonyesha tunapiga hatua. Pia tunaona maudhui sasa kwenye vyombo vya habari yameanza kubadilika, kwa kifupi kuna mtazamo chanya wa Serikali dhidi ya vyombo vya habari”.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema tangu awamu ya sita iingie madarakani imeonyesha nia ya dhati ya kuviacha vyombo vya habari vifanye kazi zake bila kuingiliwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema kuna utashi wa kisiasa katika kuvifanya vyombo vya habari kuwa huru na hilo limeonekana kwa vitendo kuanzia kwenye ushiriki wake katika mkutano uliofanyika juzi Arusha.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments