Mtoto Asimulia Dada Yake Alivyopigwa Risasi Mwanza


Picha ya Swalha Salum aliyeuawa kwa kupigwa risasi na mmewe, Said Oswayo jijini Mwanza

Mtoto mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa) amesimulia jinsi alivyobaini mwili wa dada yake, Swalha Salum (28) ukiwa kitandani ukivuja damu baada ya kupigwa risasi.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao eneo la Kirumba jijini Mwanza, mtoto huyo amesema kabla ya kuingia chumbani na kuukuta mwili huo, yeye na mwenzake waliokuwepo nyumbani muda huo walisikia milio ya risasi kadhaa.

Anasema kabla ya tukio hilo lillilotokea usiku wa Jumamosi Mei 28, 2022, marehemu dada yake na mume wake aliyemtaja kwa jina la Said Oswayo walikuwa na ugomvi huku sauti za majibizano zikisikika kutoka chumbani kwa wanandoa hao waliofunga pingu za maisha Desemba 31, 2021.

"Mimi na msaidizi wetu wa nyumbani tulikuwa tukiandaa chakula cha usiku. Tuliwasikia wakizozana kwa karibia nusu saa ndipo tikasikia milio ya kwanza ya risasi. Nilikimbilia chumbani kwao na kubisha hodi lakini hakukuwa na jibu nikaamua kuondoka," anasimulia mtoto huyo

Anasema muda mfupi baada ya milio ya kwanza ya risasi, kulisikika milio mingine na aliporejea tena kugonga mara ya pili mlango wa chumbani kwa wana ndoa hao, shemeji yake alitoka na kumtuliza kuwa hakuna tatizo na kumtaka kuendelea na shughuli zake.

"Shemeji aliniambia wana mkwaruzani kidogo kutokana na dada ambaye sasa ni marehemu kutopokea simu yake zaidi ya mara 37," anasema

Anasema baada ya maelezo hayo ya shemeji yake, aliamua kurejea jikoni lakini ghafla zikasikika milio zaidi ya risasi huku msaidizi wao wa ndani akimshauri waondoke eneo hilo, ushauri ambao aliupinga kwa kuhofia usalama wa dada yake aliyekuwa chumbani kunakosikika milio ya risasi.

"Niliporudi jikoni nikakaa kidogo tukasikia tena risasi nikatulia, nikasikia tena ya nne nikatulia jikoni ningetoka pale huenda shemeji angekuwa na hasira na mimi angenipiga, nikatulia kimya baada ya kusikia mtu anafungua mlango kuchungulia nikaona shemeji anafungua mlango akiwa ameshikilia Bastola mkononi," anasema na kuongeza

"Nilipoona hivyo niliingiwa na hofu ya usalama wa dada na kukimbilia chumbani ambako nilimkuta amelala kitandani akivuja damu nyingi,"

Anasema alikimbilia nyumba ya jirani kuomba msaada lakini walisita kufika wakidai shemeji yake ambaye ni mtuhumiwa na mauaji hayo aliwazuia majirani kuingilia migogoro kati yake na mkewe.

"Baada ya kukosa msaada kwa majirani, niliwakimblia madereva wa pikipiki ambao walitoa msaada wa kumkimbiza hospitali Bodaboda watusaidie kupiga simu polisi waliofika muda mchache na kumkimbiza hospitali.

Wakati ndugu wakielezea uwepo wa mgogoro wa muda mrefu kati ya wana ndoa hao, Chanagenge Kilosa, mmoja wa marafiki wa mtuhumiwa Oswayo ameiambia Mwananchi kuwa hajawahi kusikia taarifa zozote za ugomvi huo.

"Mimi na Oswayo tumekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka 10 sasa; sijawahi kusikia taarifa zozote kuhusu mgogoro tangu walipofunda ndoa. Hili tukio limetuacha na maswali mengi," amesema Kilosa

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mairi Makori amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ikiwemo kumsaka mtuhumiwa aliyetoweka baada ya kudaiwa kufanya mauaji hayo.

"Polisi tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ikiwemo msako dhidi ya anahetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi zaidi," amesema kaimu Kamanda huyo

Kuhusu idadi ya risasi, Kamanda Makori amesema Jeshi la Polisi litatoa taarifa za kina baada ya uchunguzi wa awali wa mwili wa marehemu kukamilika.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments