Recent-Post

Mufti Zubeir ahimiza Umoja, Ushiriki Sensa


 Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amehimiza umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu huku akiwataka kujitokeza zaidi kushiriki katika mchakato wa Sensa na Makazi utakaoanza Agosti 23 mwaka huu.

Sheikh Zubeir amesema hayo leo Jumanne Mei 3, 2022 katika swala ya Eid El- Fitr iliyofanyika kitaifa katika msikiti wa kisasa wa Mfalme Mohamed VI uliopo maeneo ya Kinondoni. Ibada hiyo imehudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine waandamizi wa Serikali wakiwemo mawaziri.

Katika hotuba yake kwa waumini wa Kiislamu Sheikh Zubeir alisema, "Tuwe na umoja na tujenge undugu zaidi kila mmoja amuone mwenzake ni ndugu na jamaa yake wa karibu ambaye ana haki ya kuheshimu.Tujenge undugu na ushirikiano miongoni mwetu ili kuangalia mbele zaidi," alisema.

Mbali na hilo, Sheikh Zubeir alizungumzia mchakato wa Sensa na Makazi akiwataka Waislamu na Watanzania kujitokeza kwa wingi kushirikia suala hilo.Alisema  ni haki kwa Waislamu na Watanzania kushiriki na kukubalia kuhesabiwa kwa  manufaa ya Taifa.

"Hili ni jambo letu sote msifuate kauli au yanayosema katika Uislamu hakuna Sensa, huyu atakuwa anajitangazia yeye ujinga kwa maneno yake.Sensa ipo mwaka huu na Serikali imeweka utaratibu mzuri.

"Ni jukumu letu viongozi wa dini kuwajibika kwa kuwaambia Waislamu na Watanzania kushiriki mchakato huu," alisema Sheikh Zubeir.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Baraza la Ulamaa la Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hassan Chizenga aliwataka waumini wa dini hiyo, kuendelea  kutoa zawadi ya Ramadhani kwa Watanzania ( akimaanisha kuendeleza kutenda matendo mema waliokuwa wakiyatenda ndani ya mwezi huo).

"Endeleeni kutoa zawadi ya tabia njema kwa kila binadamu na ulimwenguni kote.Sambazeni zawadi hizi ili viongozi wote waonekana kwa tabia njema mlizozipata ndani ya mwezi mtukufu," alisema Sheikh Chizenga.

Katika Msikiti wa Mtoro, Kariakoo, Sheikh Faraj Abdallah, alisema kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan kusiwe mwisho wa waumini wa dini hiyo kuendeleza kumtii Mungu.

"Leo ni sikukuu sio siku ya kufanya dhambia ni siku ya kumshukuru na kumtukuza Mungu kama tulivyokuwa tunafanya katika mwezi wa Ramadhani," alisema Abdallah.

Post a Comment

0 Comments