Recent-Post

Musukuma ataka wabunge wazee waende JKT

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma amehoji ni kwanini wabunge vijana tu ndio wanapewa fursa ya kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) badala ya wabunge wote wakiwemo wazee.

Musukuma amehoji hayo leo Jumatano Mei 25, 2022 alipokuwa akiomba mwongozo wa Spika baada ya Mwenyekiti wa Bunge Najma Giga kusoma fursa ya mafunzo hayo kwa wabunge vijana.

“JKT ni sehemu ya kufundishwa uzalendo na kwa vile hii taasisi ya Bunge tunahitaji kuwa na uzalendo wa hali ya juu, kwanini tunabagua wabunge vijana kwanini tusiende na wazee,”amehoji Musukuma.

Awali akiomba mwongozo wa Spika, Mbunge wa Viti Maalum Ester Bulaya amehoji kwanini mafunzo ya JKT kwa wabunge vijana yasiwe lazima ili wapiti kwa ajili ya kujengewa uzalendo na ukakamavu ili nchi iweze kuwa na askari wa akiba kuanzia bungeni hadi mtaani.

Akijibu miongozo hiyo Najma amesema kuwa kwasababu ilikuwa ni tangazo atalirudisha kwa ajili ya kutafakari vizuri jambo hilo ili ambao hawajapata nafasi akiwemo yeye waweze kwenda.

Awali Najma alitoa tangazo la fursa ya kwenda mafunzo ya JKT kwa wabunge wa vijana kujiorodhesha ili waweze kwenda kwenye mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments