Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewatahadharisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa ya majibu yenye orodha ya majina ya kazi ya muda ya sensa ya watu na makazi iliyohakikiwa na kujibiwa kikamilifu.
Taarifa hiyo ambayo imeonekana kwenye mitandao ya kijamii imetajwa kuwa ni feki na ya kupuuzwa kwani ina lengo la kuharibu zoezi hilo la kitaifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27, 2022 Mtakwimu mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema kuwa taarifa zote za majibu na usahili wa makarani na wasimamizi wa Tehama zitatolewa kupitia ngazi za mitaa na Halmashauri.
"Taarifa hizo sio rasmi kwa Watanzania walioomba nafasi za ukarani na usimamizi wa Sensa katika maeneo wanayoishi, na taarifa hiyo pia imeenda mbali na kutangaza kuwa Mei 29, 2022 kuwa tarehe ya usahili kitu ambacho si kweli," amesema.
Dk Chuwa amesema baada ya mchakato wa majibu kukamilika majibu yatatangazwa kupitia vyombo vya habari ili kudumisha uwazi na ukweli wa zoezi la sensa ya watu na makazi 2022.
Mei 5, 2022 Serikali ilitangaza nafasi za kazi za muda za makarani na wasimamizi wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 ambapo Hadi kufikia Mei 19, 2022 watu 689,935 walituma maombi ikiwa nje ya lengo la watu 205,000 waliohitajika.
0 Comments