Polisi Mbaroni Kwa Madai Ya Dawa Za Kulevya.

Vita dhidi ya mihadarati inazidi kupamba moto mkoani Kilimanjaro, baada ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), kudaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kusafirisha kilo 120 za mirungi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipoulizwa na gazeti hili juzi kuhusu tuhuma hizo, alisema taarifa anaifuatilia na hakutaka kuingia kwa undani juu ya ukamataji huo.

Awali, taarifa kutoka wilayani Rombo za askari huyo anayedaiwa kutiwa mbaroni Mei 10 mwaka huu eneo la Mengwe, zinasema alikuwa akisafirisha mirungi kwenda Babati.

Taarifa zinadai kuwa askari huyo alikamatwa akisafirisha mirungi hiyo kwa gari aina ya Toyota Corolla.

Hii ni mara ya pili kwa Polisi Kilimanjaro kuwakamata askari wake kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya. Mei 18, 2013 walimkamata EX PC George Bisongoza akisafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi.

George ambaye alikamatwa usiku wa Mei 18 eneo la Kilema Pofu Barabara ya Moshi-Himo, alikuwa akisafirisha maguni 18 ya bangi kwa kutumia gari la FFU Arusha.

Hata hivyo, George alishahukumiwa kifungo cha maisha jela Desemba 15, 2017.

“RPC Simon Maigwa, RCO na vyombo vingine vya usalama hapa kwetu (Kilimanjaro), viko makini sana. Kwenye suala hili la dawa za kulevya hawataki mchezo,” kilidokeza chanzo chetu.

“Kama unakumbuka IGP (Simon Sirro) alishaonya. Ukijiingiza kwenye mambo machafu hayo utashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Hakuna atakayekubali askari wachache wachafue jeshi linalowajibika kupambana na uhalifu.”

Katika hatua nyingine, taarifa zinadai kuwa dereva wa gari la Idara ya Afya ya Halmashauri ya Jiji la Arusha anadaiwa kukamatwa na gari hilo likiwa na shehena ya mirungi.

Hata hivyo, Kamanda Maigwa alipoulizwa na gazeti hili alisema atafuatilia taarifa hiyo.

Suala hilo la kukamatwa kwa gari linalodaiwa kuwa ni mali ya halmashauri liliibuka katika kikao cha Baraza la Madiwani, huku mkurugenzi wa jiji hilo, Dk John Pima akisema lipo chini ya vyombo vya sheria na Serikali imeshachukua hatua.

Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita ndiye aliyeliibua sakata hilo, akisema katika mitandao ya kijamii kumekuwepo na taarifa hizo, hivyo ni vyema mkurugenzi akaeleza kama taarifa za kukamatwa kwa gari hilo ni sahihi au la.

“Mheshimiwa mwenyekiti kwenye mitandao ya kijamii kumekuwepo na maneno mengi. Kuna gari la halmashauri yetu lipo Polisi Rombo kwa zaidi ya wiki sasa. Kama ni kweli ningependa jambo hili lijadiliwe kwa kina,” alisema Doita.

Akijibu hoja hiyo, mkurugenzi alisema, “hiyo taarifa nitaitolea taarifa kwenye kalenda yetu namba nane kama utaratibu ulivyo, tumepokea wageni, tuna matukio makubwa, kuna jambo lolote lile litakuwa limetokea basi tutatolea taarifa.”

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments