Rais Samia atoa ahadi ukuaji wa uchumi nchini

         

Rais Samia Suluhu Hassan amesema uchumi wa Tanzania utakua hadi kufikia asilimia 6.8 ifikapo mwaka 2025.

Rais Samia alitoa ahadi hiyo juzi jijini Accra, Ghana wakati wa majadiliano ya pamoja na viongozi wengine wa Afrika, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Majadiliano hayo yalihudhuriwa pia na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, Waziri Mkuu wa Rwanda, Edward Ngirente na Makamu wa Rais wa Ivory Coast, Tiemoko Meyliet Kone.

Akizungumza wakati akijibu swali aliloulizwa kuhusu changamoto alizokutana nazo baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alisema aliingia wakati ulimwengu ukikabiliwa na ugonjwa wa Uviko-19, jambo lililosababisha kuporomoka kwa uchumi.

Hata hivyo, aliahidi kupandisha ukuaji wa uchumi hadi kufikia asilimia 6.8 ifikapo mwaka 2025, kiwango alichokikuta wakati anaingia madarakani.

“Katika nchi yangu uchumi ulishuka kutoka ukuaji wa asilimia 6.8 hadi asilimia 4,, kwa hiyo tulikuwa na changamoto ya kuinua uchumi na hapa tunapoongea tumeanza kukua kwa asilimia 5.2 mwaka huu.

Matarajio yangu ni kurudi kwenye ukuaji wa asilimia 6.8 ifikapo mwaka 2025,” alisema Rais Samia na kuzishukuru taasisi za fedha, hususan benki ya AfDB kwa msaada ambao wamekuwa wakiipatia Tanzania katika kuleta maendeleo, hasa ya miundombinu.

Alisema Tanzania ilipata mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kukabiliana na Uviko-19, tofauti na mataifa mengine, alizielekeza fedha hizo katika kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametajwa na Jarida la Time 100 kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.

Kwa mujibu wa Time 100, Rais Samia yumo kwenye orodha hiyo kutokana na uongozi wake wa kusisimua tangu alipoingia madarakani Machi 2021 na kuleta mabadiliko makubwa Tanzania ikiwamo kufungua mlango wa mazungumzo kati ya Serikali na wapinzani wa kisiasa.

Kwa orodha hiyo, Rais Samia ameungana na marais kutoka nchi nyingine wakiwamo Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Xi Jinping wa China, Vladimir Putin wa Urusi na Joe Biden wa Marekani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments