Rais Samia mgeni rasmi miaka 10 THRDC

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) zitakazofanyika Mei 13 mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Mei 10, 2022 na Mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa wakati wa kikao kazi cha kuhakiki mpango kazi wa kitaifa wa haki za binadamu na asasi za kiraia.

“Hii ni wiki ya maadhimisho miaka 10 ya mtandao wa THRDC na kilele chake kitakuwa Mei 13 ambapo tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na wiki hii wanamtandao tunakutana kufanya vikao mbalimbali kuelekea kilele,” amesema Olengurumwa.

Amesema wanafanya tathmini ya masuala mbalimbali ikiwemo kupitia mapendekezo 187 na kuandaa mpango wa utekelezaji ni shughuli zinazofanyika kwa kushirikiana na wadau wengi.

Amesema mkutano huo utahudhuriwa na mabalozi zaidi ya 15 na taasisi mbalimnali za kimataifa, wadau kutokea Umoja wa Mataifa UN, asasi za kiraia zaidi ya 300, vyama vya kisiasa na taasisi za kidini.

Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya Development Agency, Samwel Sokoro amesema kupitia kikao kazi hicho kilichokaliwa baina yao na Serikali wataimarisha mashirikiano kwani kwa kipindi cha nyuma kumekuwa na tatizo kidogo kwenye ushirikiano huo.

“Kuyumba kwa mashirikiano kumezifanya asasi za kiraia kutotekeleza majukumu  ya kimsingi, asasi hizi zina mchango mkubwa kwenye jamii tunatarajia kufanya hizi shughuli kwa kushirikiana na Serikali.

“Baada ya mpango kukamilika na kutekelezeeka tutaweza kuifikia jamii na kushirikiana na Serikali ili wale wadau waone ni mazingira salama wao kuweka fedha zao kutekeleza miradi,” amesema Sokoro.

Everine Lyimo kutoka asasi ya Save the mother and children iliyopo Singida amesema, “Tunatarajia kufanya kazi pamoja na Serikali hasa Singida kwa sisi watetezi wa haki za wanawake na watoto katika mkoa wa Singida tunahitaji ushirikiano wa bega kwa bega.”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments