Sakata La Bei Ya Mafuta… CCM Yatoa Maagizo, Serikali Yatekeleza

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kukabiliana hali ya maisha iliyopo kwa sasa nchini inayotajwa kuchangiwa na kupaa kwa bei ya mafuta.

Bei ya dizeli na petrol imezidi kupaa na sasa imefikia Sh3,264 kwa lita huku petrol ikiwa ni Sh3,148 kwa Jiji la Dar es Salaam huku baadhi ya mikoa bei ikiwa juu zaidi kutokana na umbali.

Hatua hiyo imesababisha bei za bidhaa nyingine muhimu ikiwemo vyakula kupaa kwa kasi hivyo, kuongeza ugumu wa maisha kwa mwananchi wa kawaida jamboa ambalo limeilazimu CCM kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka.

Hata hivyo, agizo hilo la CCM limekuja wakati Serikali ikitarajiwa kutoa kauli kuhusu bei za mafuta na masuala mengine muhimu kuhusu mwenendo wa maisha na uchumi kwa ujumla. Taarifa hiyo itatolewa bungeni Jumanne ya Mei 10, 2022 na Waziri mwenye dhamana ya nishati, January Makamba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, iliyotolewa  leo Jumatatu Mei 9, 2022 imesema kuwa CCCM imeguswa na hali ya maisha ilivyo kwa wananchi na kuiagiza Serikali kuchukua hatua.

“Kufuatia hali hii Chama kimeielekeza Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kukabiliana nayo ili kuwapunguzia wananchi makali ya maisha. “Tunafanya hivyo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zetu kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo tuliahidi kuisimamia serikali ili kuwaletea maendeleo Watanzania na kuimarisha ustawi wao,” imesema taarifa hiyo ya Shaka na kuongeza:

“Pamoja na sababu za kitaalamu zinazotajwa kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta na kupelekea mfumuko huu wa bei nchini, CCM iko makini na inafuatilia mwenendo mzima. Kimesema kuwa Chama hakiwezi kukaa kimya wakati wananchi wake wakiwa kwenye changamoto hivyo, lazima Serikali ichukue hatua na kuwaeleza wananchi nini kinafanyika kukabiliana na hali hiyo ili kuwapa wananchi unafuu wa maisha.”

Kupitia taarifa hiyo, Shaka pia amewaomba Watanzania kuwa watulivu na kuendelea kuiamini Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo tayari imeahidi kuchukua hatua bila kuathiri shughuli zingine za maendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya CCM kutoa taarifa yake hiyo, Rais Samia ametoa taarifa akisema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo. Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari muda mfupi uliopita, Rais Samia amesema kuwa kuanzia Juni 1, 2022 bei ya mafuta itashuka ili kutoa nafuu kwa wananchi.

Hata hivyo, amesema kuwa taarifa ya kina kuhusu masuala mbalimbali ya bei ya mafuta na kupanda kwa bidhaa na hatua zinazochukuliwa na Serikali itatolewa na mawaziri husika: Mwigulu Nchemba (Fedha na Mipango) na Januari Makamba (Nishati).

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments