Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga leo Jumatano Mei 25,2022 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.
Mbunge huyo alisema wakati mwingine mwanafunzi anapofanya mitihani ya mwisho anakuwa amechanganyikiwa.
Akahoji kwanini sasa Serikali isiangalie mitihani yake ya nyuma ili kumhukumu mwanafunzi kwa maisha yake ya baadaye.
Akijibu swali hilo Kipanga alisema mtihani wa mwisho kwa wahitimu wa kidato cha nne sio pekee yanayozingatiwa katika matokeo ya kidato cha nne.
Alisema wahitimu wamekuwa wakipimwa ufaulu wao kwa kutumia asilimia 30 ya maendeleo yao ya elimu ya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na asilimia 70 ni ya mitihani yao ya mwisho.
Katika swali la msingi Mbunge wa Kibaha Vijijini (CCM), Costanino Mwakamo amehoji Serikali imejipangaje kuwaendeleza vijana wanaomaliza kidato cha nne na kupata daraja la nne au sifuri
Akijibu swali hilo Kipanga amesema Serikali imetoa fursa kwa vijana wote hata wale waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Pia amesema wanafunzi hao wamepewa fursa ya kujiunga na vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo karibu na maeneo wanayoishi kwa lengo la kujiendeleza katika ujuzi na stadi mbalimbali za maisha.
“Vijana hao wanaweza kurudia mitihani yao kama watahiniwa wa Kujitegemea iwapo wanahitaji kufanya hivyo,”amesema.
Amesema pia wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu inatekeleza programu ya kukuza ujuzi kwa kuwapatia vijana mafunzo ya uanagenzi na utambuzi wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.
0 Comments