SERIKALI YAOMBWA GARI LA ZIMAMOTO MIRERANI

Serikali imeombwa kuwepo na gari la zimamoto kwenye Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ili kuweza kunusuru majanga ya moto pindi yakitokea.


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Yusto Gabriel Mlay ameyasema hayo kwenye zoezi la utayari la kupambana na moto pindi ukitokea lililofanyika kwenye jengo la Benki ya NMB Mirerani.

Mlay amesema mji mdogo wa Mirerani unazidi kukua hivyo kunapaswa kuwe na gari la zimamoto pindi kukitokea majanga ya moto.

"Gari la zimamoto ni muhimu kwani Mirerani ni mji unaokuwa kwa kasi, kuna taasisi mbalimbali za Serikali, kuna migodi ya Tanzanite na ukuta unaozunguka migodi," amesema Mlay.

Hata hivyo, amesema lengo la kufanya zoezi hilo la moto kwenye jengo la NMB Mirerani ni kuona utayari wa watu pindi janga la moto likitokea.

"Watu walishtuka na kudhani ni ajali ya moto kweli ila tuliwashirikisha namna ya kuzima moto pindi ajali ikitokea hivyo wafanyakazi na majirani zao wamepata elimu ya kuzima moto," amesema Mlay.

Mmoja kati ya walioshuhudia utayari huo Rose Mollel amesema awali alidhani ni ajali ya moto imetokea ila akajulishwa ni zoezi la utayari.

"Mimi ni mteja nilifika benki ya NMB kwa ajili ya kuhifadhi fedha ila kupitia zoezi hili la utayari nami nimepata elimu ya kuzima moto pindi ukitokea," amesema.

Mkazi wa Mirerani Aloyce John amesema kuwepo kwa gari la zimamoto itakuwa ni hatua nzuri ya kwani changamoto hiyo ni ya muda mrefu.

Amesema hivi karibuni kuna nyumba iliungua pembeni ya barabara kuu ya Kia-Mirerani japokuwa askari wa zimamoto walipambana isisababishe nyumba nyingine kuungua.

"Hata mwaka 2017 kulitokea ajali ya moto kwenye moja kati ya mgodi uliopo kitalu B 'Opec' na ukateketea kutokana na kukosekana kwa gari la zimamoto," amesema John.

Na Mwandishi wetu, Mirerani

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments