Recent-Post

Tembo Wameshaua Watu 60 Tangu Mwanzoni Mwa Mwaka Huu Nchini Zimbabwe

Raia 60 wa Zimbabwe wameshauliwa na tembo hadi hivi sasa tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022. Hayo yalisema jana na msemaji wa serikai ya nchi hiyo na kuongeza kuwa, ugomvi baina ya wanadamu na wanyamapori unazidi kuongezeka kutokana na kupungua maeneo ya wanyama hao nchini humo.

Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa kuna ndovu 100,000 nchini Zimbabwe idadi ambayo inahesabiwa ni ya pili kwa ukubwa duniani baada ya ile ya Botswana. Idadi ya tembo walioko Zimbabwe ni robo nzima ya tembo wote walioko duniani.

Tofauti na maeneo mengine ambako majangili wameua tembo wengi kwa ajili ya pembe zake, ujangili unaonekana si mkubwa huko Zimbabwe kwani takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hao inaongezeka kwa asilimia tano kila mwaka.

Msemaji wa serikai ya Zimbabwe, Nick Mangwana ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, katika baadhi ya maeneo, ndovu wamevamia mashamba ya watu na kuharibu kabisa mazao na hivi sasa makundi ya wanyama hao yanaelekea kwenye makazi ya watu na kuwalazimisha wakazi wa maeneo hayo kuchukua hatua.

Baadhi ya ndovu wamekuwa wakiwashambulia watu, wengine wakiwajeruhi na wengine wakiwaua. "Wakati tembo anapojeruhiwa huwa na hasira na hazuiliki wala hadhibitiki tena," amesema.

Aidha amesema, ugomvi baina ya wanadamu na wanyamapori limekuwa ni tatizo kubwa hivi sasa. Katika mwaka huu pekee na ikiwa imepita miezi michache tu tangu uanze mwaka 2022, tayari Wazimbabwe 60 wameshauliwa na ndovu na wengine 50 wameshajeruhiwa.

Amekumbusha kuwa, mwaka uliopita wa 2021 idadi yote ya watu waliouliwa na tembo nchini Zimbabwe ilikuwa ni 72. Wanyama hao wamekuwa wakitangatanga nje ya hifadhi za taifa kutafuta chakula.

Post a Comment

0 Comments