TUME YA MADINI YAENDELEA KUWAPIGA MSASA WADAU WA MADINI KUHUSU USHIRIKISHWAJI KATIKA SEKTA YA MADINI

Tume ya Madini imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia Jukwaa la Kwanza la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea jijini Mwanza.

 
Jukwaa hilo la siku tatu linaloambatana na maonesho lililoanza mapema jana tarehe 20 Mei, 2022 linakutanishwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wachimbaji wa madini, watoa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mabenki, na watendaji kutoka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini.
 
Mada mbalimbali zilizowasilishwa ni pamoja na changamoto na malengo katika ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini, fursa na changamoto zilizopo katika ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini.
 
Majadiliano yaliyofanyika yamelenga katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na ulinganifu wa manufaa na maendeleo ya ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini kabla na baada ya kuanzishwa kwa kanuni za ushirikishwaji  wa watanzania mwaka 2018 na changamoto za watoa huduma kwa wamiliki wa leseni za madini na namna ya kuzitatua.
 
Akizungumza katika jukwaa hilo mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ringo Iringo amewataka watoa huduma kwenye migodi ya madini kuungana kwa pamoja ili kufanikiwa kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi hasa ikizingatiwa huduma zinahitaji mitaji mikubwa.
 
“Kuna huduma nyingine muhimu kwenye migodi ya madini zinahitaji mitaji mikubwa hivyo nashauri watoa huduma kuunganisha nguvu kwa pamoja, wenye fedha na teknolojia na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa,” amesema Iringo.
 
Katika hatua nyingine amewataka sambamba na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa kuwa na utamaduni wa kufanya utafiti juu ya teknolojia mpya zinazotumika kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini ili kuweza kuingia kwenye soko la ushindani kimataifa.
 
Jukwa hilo linatarajiwa kufungwa kesho na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko.













TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments