TUNAENDA KUONDOA MACHUNGU YETU YA MSIMU HUU - SIMBA SC

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wamesema kuwa wanaenda kuikabili Yanga SC katika mchezo wa Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 28, 2022 katika dimba la CCM Kirumba, Mwanza wakitaka kufuta machungu ya msimu huu ambapo wanaelekea kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.

Akizungumza jijini Mwanza, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amesema Simba SC ina lengo la kuchukua ubingwa wa ASFC wakati Yanga SC wana lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu.

“Kombe la Mapinduzi tulichukua kule Zanzibar, lakini kwenye Ligi Kuu mambo magumu, huku kwenye ASFC, kila mtu kajiandaa lakini sisi hatuna cha kupoteza katika mchezo huo wa Jumamosi, tuna nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe hili”, amesema Ahmed.

Pia amesema watakuwa wamefika asilimia 70% msimu huu wa mashindano kwa kuchukua Kombe la Mapinduzi na hata la Kombe la ASFC endapo watafanya hivyo, amejivunia kwa Simba SC kutawala Soka la Tanzania katika kipindi cha miaka minne.

“Katika kipindi cha miaka minne hatujawahi kufeli katika Michuano hii ya ASFC, tumewafunga watu wengi katika hatua muhimu wakiwemo Yanga SC wenyewe tumewafunga kwenye Nusu Fainali, hata Fainali tumewafunga pia”, ameeleza Ahmed.

Kuhusu majeruhi ya Wachezaji wao, amesema Golikipa wa timu hiyo, Aishi Salum Manula aliumia baada ya kukatwa na Kioo katika Vidole vyake viwili, hali yake inaendelea vizuri wakati akiuguza kidonda, licha ya Aishi kuumia, amesema wana Kipa mwengine Beno Kakolanya.

“Majeruhi Clatous Chama tumekuja naye hapa Mwanza na alikuwa anafanya mazoezi peke yake (binafsi) na hali yake inaendelea kuimarika zaidi wakati tukijiandaa na mchezo huo wa Nusu Fainali ya Michuano ya ASFC”, amesema Ahmed.

Hata hivyo, amesema Mlinzi wa Kulia wa timu hiyo, Shomari Kapombe aliumia ‘Nyama za Paja’ katika mchezo dhidi ya Geita Gold FC, pia na yeye anaendelea na mazoezi na kuimalika kidogo kidogo.

Post a Comment

0 Comments