Vikosi vya Israel vyawashambulia waombolezaji waliobeba jeneza la mwandishi wa Al-Jazeera


 Vikosi vya Israel vimeushambulia umati wa waombolezaji waliokuwa wamebeba jeneza la mwandishi wa habari wa Al Jazeera aliyeuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akiripoti uvamizi katika Ukingo wa Magharibi mapema wiki hii.

Mwili wa mwandishi huyo, Shireen Abu Akleh ulikuwa ukipelekwa kutoka katika mji wa Jenin - ambako aliuawa na vikosi vya Israel, kwa mujibu wa mashahidi - hadi Jerusalem kupitia Nablus na Ramallah, katika maandamano kabla ya mazishi yake katika Jiji la Kale la Jerusalem Mashariki.

Hata hivyo, waombolezaji, wengi wao wakiwa wamebeba bendera za Palestina, wakisafirisha jeneza la mwandishi huyo wa habari Mpalestina mwenye asili ya Marekani kutoka Hospitali ya St. Louis ya Ufaransa katika kitongoji cha Sheikh Jarrah, walishambuliwa na vikosi vya usalama vya Israel.

Kanda za video zilizosambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zilionyesha maofisa wa Israel waliokuwa na silaha wakiwashukia wale waliokuwa wakitembeza jeneza wakiwa na bakora, kabla ya kuwapiga baadhi ya waombolezaji.

Pia, kulikuwa na ripoti za maguruneti yaliyotumiwa. Miongoni mwa wale waliokimbia eneo la tukio walikuwa watoto na wanawake, huku wajumbe wengine wa msafara wa Abu Akleh wakijaribu kulinda jeneza lake ambalo linaonekana kukaribia kuanguka chini katika baadhi ya maeneo.

Katika shambulio la Jumatano iliyopita, mwandishi mwingine wa habari, anayefanya kazi na gazeti la Al-Quds la Jerusalem, pia alipigwa risasi na kujeruhiwa katika tukio hilo, na pia aliilaumu Israel kwa tukio hilo.

Awali, jeshi la Israel lilipinga kuwa vikosi vyake viliwapiga risasi waandishi hao wawili wa habari. Lilisema wanajeshi wa Israel walishambuliwa kwa milio ya risasi na vilipuzi walipokuwa wakifanya kazi huko Jenin na kwamba walifyatua risasi kujibu.

Jeshi hilo  lilisema linachunguza tukio hilo na kuangalia uwezekano kwamba waandishi hao walipigwa na wapiganaji wa Kipalestina.

Israel sasa imetaka uchunguzi wa pamoja na Mamlaka za Palestina kuhusu mauaji hayo. Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas amesema kuwa atapeleka kesi ya Abu Akleh katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu katika juhudi za kupata haki kwa mwandishi huyo.

By Peter Elias

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments