Viongozi wa Umoja Wa Afrika Wanakutana Malabo Kujadili Usalama Wa Chakula, Ugaidi


Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanakutana katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta, Malabo kujadili masuala ya usalama wa chakula, ugaidi na mapinduzi ya kijeshi katika bara hilo.

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanakutana katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta, Malabo kujadili masuala ya usalama wa chakula, ugaidi na mapinduzi ya kijeshi katika bara hilo.

Mkutano huo wa siku mbili umefunguliwa Ijumaa huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni. Kati ya watu bilioni 1.4 barani Afrika, takriban milioni 282 wanakabiliwa na utapiamlo. Aidha maeneo ya Sahel na Pembe ya Afrika yanakabiliwa na baa la njaa kutokana  na mabadiliko ya hali ya hewa, vitendo vya kigaidi, na migogoro ya kijamii.

Siku ya Ijumaa wafadhili walishiriki kwenye mkutano huo wa kilele wa kwanza na wa kipekee uliolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya kibinadamu.

Kwenye taarifa, Umoja wa Afrika umesema nchi 15 ambazo zimeathiriwa mno zinahitaji misaada ya dharura hasa wakati huu ambao athari za mabadiliko ya tabia nchi zinayafanya mahitaji ya kibinadamu yaongezeke kwa kiwango kikubwa.

Umoja huo umeongeza kuwa miongoni mwa watu milioni 30 ambao wamepoteza makaazi yao, zaidi ya milioni 10 ni watoto walio na miaka chini ya 15, na sababu ya hali hiyo imetajwa kuwa ni mizozo ya kikabila katika baadhi ya kanda na vilevile tatizo la ukosefu wa upatikanaji wa chakula.

                     

Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO limesema takriban watu milioni 282 miongoni mwa idadi jumla ya watu barani Afrika Bilioni 1.4, hawapati chakula cha kutosha. Hiyo ikiwa ni ongezeko la watu milioni 49 tangu mwaka 2019.

Katika kikao cha leo Jumamosi viongozi wa Afrika wanajadili njia za kukabiliana na ugaidi pamoja na mapinduzi ya kijeshi.

Nchi kama vile Libya, Msumbiji, Somalia, Eneo la Sahel, Ukanda wa Ziwa Chad, na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni maeneo ya Afrika ambayo yanakumbwa na uasi na hujuma za kigaidi na hivyo wakuu wa Umoja wa Afrika wanatazamiwa kutafutia njia za kukabiliana na hali hiyo.

Aidha viongozi wa Umoja wa Afrika leo wanajadili mapinduzi ya kijeshi ya miaka ya karibuni huko Mali, Guinea, Sudan na Burkina Faso.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments