Wabunge 19 Waliofukuzwa Chadema Watinga Bungeni, Mmoja Auliza swali

Baadhi ya wabunge kati ya 19 wa Viti Maalum waliofukuzwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameingia bungeni kuendelea kushiriki vikao vya Bunge.

 Aliyeingia wa kwanza kuingia bungeni leo Jumatatu Mei 16, 2022 ni Sophia Mwakagenda ambaye aliingia kwa kutumia mlango wa kawaida akiwa ameongozana na wabunge wengine wa CCM na moja kwa moja kaingia ukumbini.

Mwakagenda kaingia viwanja vya Bunge saa 2.44 asubuhi akitumia geti la kawaida ambalo hutumiwa na wabunge wote.

Dakika sita baadae waliingia Grace Tendega na Conchesta Rwamlaza ambao wao walitumia mlango wa geti linalotumiwa na watumishi wengine maarufu geti la Waziri Mkuu

Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega akiuliza swali bungeni leo Jumatatu Mei 16, 2022

Muda mfupi baada ya kuanza shughuli za bunge, waliingia Taunza Malapo na Cecilia Pareso na kama ilivyo kwa wenzao walikaa kwenye Viti vyao na kila mmoja alifungua kishikwambi chake kufuatilia shughuli za bunge ambazo hutumiwa kidigitali kwenye vishikwambi.

Kwenye kipindi cha maswali Grace Tendega alipewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kuhusu ukubwa wa Jimbo la Kilolo akihoji ni lini Jimbo hilo ligawanywa kiutawala kwani ni kubwa.

Swali hilo limejibiwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi David Silinde akiomba wahusika wafuate taratibu zinazotakiwa na Serikali itakapojiridhisha italigawa Jimbo hilo.

Wengine walioingia bunge likiendelea ni Jeska Kishoa, Nusrat Hanje na Ester Matiko.

Ndani ya Bunge Jeska Kishoa alionekana akipita kwenye viti walivyokaa wenzake na kuwaonyesha simu yake kama kitu kilichokuwa kimeandikwa ili wasome.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments