Waitara adai mawaziri waliokwenda kutatua mgogoro Mara waliishia ofisi ya RC

 Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema mawaziri wanane waliokwenda kutatua migogoro ya ardhi, hawakwenda katika maeneo ya migogoro bali waliishia ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Mawaziri waliokuwa katika kamati ya mawaziri nane ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa (Tamisemi).

Nyingine ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Maji na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano.

Waitara ameyasema hayo leo Alhamis Mei 26, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2022/2023.

“Wamekwenda pale wamejifungia ofisini mheshimiwa mwenyekiti hiyo sio sawa. Hawakwenda kwenye maeneo yenye migogoro kuwasikiliza wananchi ambao wameishi pale zaidi ya miaka 70,” amesema.

Ametaka Bunge litoe muda wa mawaziri hao kushughulikia migogoro ya wananchi na kupeleka taarifa katika junge juu ya utatuzi wa migogoro hiyo ambayo imekuwa ikisababisha vifo.

Waitara amesema ni vyema wamalize migogoro hiyo kabla ya uchaguzi maana wakienda wakati wa uchaguzi wananchi wanaona kuwa wamefika kwa ajili ya hiyo.

Post a Comment

0 Comments