Waumini 800 Washiriki Kongamano Kumuombea Rais Samia, Taifa

Waumini zaidi ya 800 wa madhehebu mbalimbali ya dini wanashiriki kongamano la kuliombea Taifa na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan linalofanyika leo huku wakisisitiza amani, utulivu na utengamano wa kisiasa na kiuchumi.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Mei 31, 2022,  Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Ayasi Njalambaa amesema kuwa viongozi wa dini walikutana na kuona namna bora ya kutenga siku maalumu   kumpongeza  Rais Samia Suluhu kwa kufanya maombi yatakayo ambatana na  kongamano kubwa la kumshukuru Mungu kwa utendaji wake na alipolifikisha Taifa.

''Tumeona Rais Samia amepitia kipindi kigumu cha uongozi wake na pia kafanya mambo makubwa ya kugusa nyanja mbali mbali za kiuchumi na kupelekea kushangaza mataifa mengine kwa kiongozi Mwanamke kufanya mambo makubwa''amesema.

Kwa upande wake Askofu  Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu  Gervas Nyaisonga amesema kongamano hilo linalenga  kumshukuru Mungu na kuwaombea viongozi wakuu wa nchi na Rais Samia Suluhu Hassan ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uwepo wa Mungu.

''Kama walivyozungumza viongozi wengine wa dini mashekhe na Mufti kuwa kongamano hili lengo ni kuliombea Taifa na viongozi wake kila jambo la baraka kwa viongozi wakuu wa nchi linahitaji nguvu ya maombi  ili kuweza kufanikiwa  ni lazima viongozi wa dini tushikamane katika kufanya maombi '' amesema.

Naibu Muft Mkuu Zanzibar, Mohamed Mussa amesema “Mama yetu Rais Samia ni Rais mwenye bahati, bahati ya kwanza alipigiwa kura na Watanzania wakati akiwa Makamu wa Rais, bahati ya pili Katiba imemchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya hayati Rais John Magufuli kufariki dunia”.

"Mimi ni miongoni mwa wadau wa  hayati Magufuli,  alimuamini Mama yetu Samia Suluhu Hassan mara mbili awe msaidizi wake, kama yeye alimuamini mimi na wewe kwanini tuwe na nongwa  ''amesema

Mwenyekiti wa  kamati ya ushauri wa Makanisa ya Pentekosti, Askofu Dk Donald Mwanjoka amesema kuwa kongamano hilo limelenga kumshukuru Mungu na  kuliombea taifa amani  kwa  kutekeleza kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu ya kazi iendelee.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano  Mkoa wa Mneya, Oscar Hongere amesema maombi ya pamoja yanampa Mungu nafasi ya kuinua Taifa la Tanzania na viongozi wakuu wa nchi  kufanikiwa katika nyanja zote kiuchumi.

Amesema kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kulipeleka taifa mbele za Mungu na kwani maombi na dua zimekuwa zikisikika mbele za  Mungu kuleta majibu kwa watanzania. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments