YANGA SC YATAJA SABABU ZA KUWEKA KAMBI SHINYANGA

WANANCHI! Yanga SC wametaja sababu za kutoka nje ya jiji la Mwanza na kuweka kambi mkoani Shinyanga, wakidai Simba SC walichukua viwanja vyote vya mazoezi katika jiji hilo la Rock City.

Akizungumza jijini Mwanza, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Hassan Bumbuli amesema Viongozi wa Simba SC waliweka oda (booking) viwanja vya Nyamagana, Butimba, na Misungwi, ndio maana Kikosi hicho kimeenda kuweka kambi mkoani Shinyanga.

Bumbuli amesema Yanga SC haijatolewa mchezoni kukosa viwanja hivyo jijini Mwanza, huku akisema huo ni utamaduni wa timu hizo. Amesema, “Timu moja inapoweka kambi sehemu moja basi nyingine inatoka eneo hilo kutafuta sehemu nyingine kwa ajili ya kambi hiyo, Utamaduni huo upo siku zote”.

“Tunajua wamewekeza wasiondoke hivi hivi msimu huu, mashabiki njooni CCM Kirumba tutatoka kifua mbele lakini msije na matokeo yenu mfukoni, tunaamini tuna Kikosi kizuri cha ushindani tumecheza michezo mingi bila kupoteza katika Ligi”, amesema Bumbuli.

Bumbuli amesema siku ya Jumamosi, Simba SC watajiuliza kwa nini wamepata sare mbili katika michezo miwili ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, amesema safari hii Simba SC hawatoki katika mchezo huo wa Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la ASFC.

Pia amesema kwa rekodi, Yanga SC wanajivunia kuwafunga Simba SC mara nyingi katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza toka enzi na enzi, licha ya kukubali rekodi nzuri ya Simba SC katika Michuano hiyo miaka ya hivi karibuni wakikumbuka kipigo cha mabao 4-1 katika mchezo wa Nusu Fainali ya Michuano hiyo.

Yanga na Simba SC watakutana kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya Michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) msimu huu, Mei 28, 2022 katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza majira ya Saa 9:30 Alasiri.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments