Zitto: Nakerwa Kuitwa Msaliti Wa Mageuzi

Tuhuma za usaliti zinazoibuka mara kwa mara kwenye vyama vya siasa kwa namna moja au nyingine zimechangia kuviumiza vyama na wanaobebeshwa tuhuma hizo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ni miongoni mwa waliokumbana na tuhuma za kufanya usaliti kwa kuandaa mapinduzi ya uongozi akiwa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Siku chache zilizopita akiwa kwenye maadhimisho ya miaka minane tangu kuanzishwa kwa ACT-Wazalendo, Zitto alizungumzia tuhuma za usaliti zinavyoathiri ukuaji wa vyama vya siasa na wanasiasa wanaolengwa.

Akizungumza na Mwananchi wakati wa mahojiano maalumu jijini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto, aliyewahi kuwa mbunge wa majimbo ya Kigoma Kaskazini na mjini kwa nyakati tofauti anakana tuhuma hizo, akisema hawezi kusaliti demokrasia na mageuzi ambayo yeye ameyapigania tangu akiwa na umri wa utoto.

“Mimi ni miongoni mwa watu tuliopachikwa jina la usaliti, kama binadamu, siwezi kujisikia vizuri kuitwa msaliti wa mageuzi na demokrasia kwa sababu tu nasimamia kile ninachokiamini ambacho wenzangu hawakubaliani nacho.”

Zitto anasema tuhuma hizo msingi wake ni watu kushindwa kukubali ukweli kila mtu ana mtazamo na msimamo juu ya jambo fulani.

“Hata hivi sasa ninapotofautiana na vyama vingine vya upinzani kuhusu nini kitangulie kati ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi bado ninaonekana ni msaliti, jambo ambalo si sahihi hata kidogo,” anasema.

“Pengine tatizo langu linalosababisha kupachikwa majina mabaya, ikiwemo la usaliti ni kufikiri tofauti na wenzangu kuhusu namna bora ya kufikia mafanikio kwenye jambo tunalolipigania. Lakini kinachonipa faraja ni kwamba mwisho wa siku tunajikuta tutakuwa na msimamo wa pamoja katika kilekile kilichosababisha niitwe msaliti,” anasema Zitto.

Huku akizungumza kwa hisia na utulivu, mwanasiasa huyo kijana aliyeanza harakati za kisiasa akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema baadhi ya wanaomwita mnafiki hadharani kwa sababu tu anatofautiana nao kimsimamo, huunga mkono hoja zake wanapozungumza faragha.

“Wapo ambao hadharani wanapinga msimamo wa ACT-Wazalendo wa tume huru kuelekea Katiba mpya. Lakini pembeni wanatuunga mkono kwa sababu wanajua ni rahisi kupata tume huru kwa kurekebisha sheria kulinganisha na mchakato wa Katiba mpya unaopitia mlolongo mrefu ukiwemo kura ya maoni,” anasema.

Chaguzi zijazo

Anasema bila tume huru, uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utasimamiwa na tume ya uchaguzi ya sasa anayodai haiko huru kimuundo na uteuzi.

Anasema kutokana na umuhimu wa tume huru na Katiba mpya, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimegawa jukumu la kudai mambo hayo kwa Baraza lake la Vijana (Bavicha) na lile la Wanawake (Bawacha).

“Bawacha wamekabidhiwa kazi ya kudai tume huru ya uchaguzi huku Bavicha wakipigania Katiba mpya, wao Chadema wanapigania mambo haya mawili muhimu kwa pamoja. Lakini sisi tumechagua kupigania kwanza tume huru na baadaye Katiba mpya. Kosa letu liko wapi?” anasema na kuhoji

Kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu na Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge waliwaambia wajumbe wa kikao cha kamati ya utendaji ya Chadema Kanda ya Victoria kilichofanyika jijini Mwanza Juni mwaka jana kuwa vipaumbele vya mabaraza hayo katika kipindi cha miaka minne ni ajenda ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

“Chadema wanapigania Katiba mpya na tume huru kwa pamoja na sisi ACT-Wazalendo tumechagua kuanza na tume huru, basi ni vema kila chama kisukume kwa nguvu ajenda yake. Sisi ACT-Wazalendo tusukume tume huru na Chadema wasukume kwa pamoja katiba mpya na tume huru. Hakuna tatizo katika hili,” anasema na kuongeza:

“Mimi binafsi na chama changu hatutasita wala kuona aibu kuisimamia na kuitetea hoja ya tume huru ya uchaguzi; wenzetu nao wasukume hoja na ajenda nyingine ili hatimaye tufikie kwenye malengo yetu ya pamoja. Tusimamie kanuni ya kutogombana kwenye jambo ambalo mwisho wa siku linatuweka pamoja”.

Akijibu swali la kwa nini watu wanapinga msimamo huo licha ya kujua ukweli, Zitto anasema: “Tatizo linalotukabili kama jamii ni tabia ya baadhi ya watu kuishi kwa kufuata upepo badala ya kusimamia kile wanachokiamini. Mimi siko hivyo. Naamini na kutetea kile nilicho na uhakika nao bila kupuuza mawazo, maoni na misimamo ya wengine.”

Wabunge 19

Akijibu swali iwapo chama chake kitakuwa tayari kuwapokea wanachama wapya wakiwemo wabunge 19 wa viti maalumu ambao Chadema ilitangaza kuwavua uanachama, Zitto anasema; “ACT-Wazalendo hatuwezi kukataa kupokea wanachama wapya; chama cha siasa kinachokataa kupokea wanachama wapya hakiwezi kukua.”

Uamuzi wa wabunge hao kuvuliwa uanachama na nyadhifa zote za uongozi ulitangazwa Novemba 27, 2020 na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema ni maamuzi ya Kamati Kuu.

Desemba Mosi, 2020, Wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, wabunge hao walitangaza kukata rufaa Baraza Kuu la Chadema linalotarajiwa kukutana leo Mei 11, huku hatima ya wabunge hao ikiwa miongoni mwa ajenda.

Uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kuwavua uanachama wabunge hao ulitokana na madai ya wao kukiuka msimamo wa chama wa kutotambua matokeo ya uchaguzi wa 2020 kwa kukubali kuapa bungeni.

Pamoja na Mdee, wengine waliovuliwa uanachama ni aliyekuwa makamu wake Hawa Mwaifunga (Bara), aliyekuwa katibu mkuu Bawacha, Grace Tendega, manaibu wake Jesca Kishoa (Bara) na Asia Mohammed (Zanzibar) pamoja na aliyekuwa mwenezi wa baraza hilo, Agnestar Lambert.

Wengine ni Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Nusrati Hanje, Tunza Malapo, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Ester Matiko na Conchesta Rwamlaza.

“Utayari wa ACT-Wazalendo wa kuwapokea haumaanishi kwamba tunakubaliana na njia walizotumia kupata ubunge. Ni dhahiri walikiuka kanuni za siasa ikiwemo uwajibikaji wa pamoja katika maamuzi ya vikao na misimamo ya kitaasisi,” anafichua Zitto.

“Licha ya mambo waliyoyafanya, haiondoi dhamira yao ya kufanya siasa, kwani watu hukosea na kujirekebisha wakipewa nafasi. Wakija tutawapokea.”

Hata hivyo, kiongozi huyo wa chama anasema kabla ya kupokewa, wabunge hao watalazimika kuthibitisha utayari wao wa kuendelea kufanya siasa na kuendeleza harakati za kupigania yale wanayoyaamini kwa sababu miongoni mwa wabunge hao, wapo ambao hawatiliwi shaka imani yao katika mabadiliko na demokrasia.

“Kuna maswali ya kujiuliza na kupata majibu yake, ikiwemo iwapo bado wanataka kufanya siasa au wanaotaka tu ubunge,” anasema.

Maoni ya mdau

Edwin Soko, mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini anasema ni kete muhimu kisiasa kwa ACT-Wazalendo kuwapokea wabunge hao iwapo Chadema itashikilia msimamo wa kuwavua uanachama.

“Licha ya makosa yao, ni ukweli kwamba miongoni mwa wabunge wale kuna viongozi wa juu na wapambanaji mahiri wa Chadema. Huu ni mtego ambao Chadema lazima wautegue kwa aidha kutoa msamaha kama wenzao CCM walivyotoa kwa akina Bernard Membe, Sophia na wengine kadhaa waliofukuzwa na kurejeshwa au washikilie uamuzi wa kuwafukuza,” anasema Soko.

Anasema msimamo wa kuwafukuza, itailazimisha Chadema kuwaandaa makada wengine wenye uwezo wa kuziba pengo lao kuendeleza mapambano ya demokrasia, kazi anayoamini itachukua kipindi kirefu kukamilika.

Matarajio 2025

“ACT-Wazalendo kama taasisi ya siasa tunafanya harakati na kampeni za kujiimarisha inayolenga kufikisha chama kila kona ya nchi Tanzania Bara na Zanzibar. Mikakati hii inatupa matarajio ya kushinda chaguzi zijazo kuanzia ule wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025,” anasema.

Huku akifichua matamanio yake ya nafasi ya urais wa Tanzania, Zitto anasema kwa mikakati inayojiwekea ACT-Wazalendo, anasema chama chake kimejipanga kuanzia nafasi nyingi za wenyeviti na wajumbe wa Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na urais na hatimaye kuongoza dola.

Anasema katika mukhtadha wa kujiimarisha, viongozi wa juu wa chama hicho walipiga kambi ya siku kadhaa jijini Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kutekeleza kampeni kushawishi wanachama wapya, hii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya chama hicho kutimiza miaka minane tangu kianzishwe.

Akizungumzia mikakati ya ACT-Wazalendo ya kujiimarisha kisiasa na ndoto ya Zitto ya Urais, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na wakili wa kujitegemea jijini Mwanza, Majid Kangile anasema kwenye siasa hakuna kisichowezekana iwapo chama na wagombea wataweka mikakati madhubuti, kuandaa na kunadi sera zinazovutia wapigakura.

“Kila chama chenye usajili wa kudumu kina haki ya kushiriki, kushinda uchaguzi na kuongoza dola. Hata Zitto pia ana haki ya kugombea Urais kwa sababu anazo sifa. Jambo muhimu ni yeye na chama chake kuwa na sera za kushawishi wapigakura ambao pia watawapima kwa ahadi na historia yao ya uongozi na utendaji katika nafasi walizowahi kushika.”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments