AWAMU YA KWANZA YA WAKAZI WA NGORONGORO WAANZA SAFARI KUHAMIA HANDENI TANGA...RC ARUSHA ATOA KAULI

Hatimaye  Historia imeandikwa! Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya wakazi waliokuwa wanaishi Ngorongoro kuamua kuanza kuondoka kwa hiyari yao kuelekea Kijiji Cha Msomela wilayani Handeni Mkoa wa Tanga ikiwa ni hatua ya kuunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuwaomba kupisha eneo la hifadji ya Ngorongoro kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania na Dunia kwa ujumla.


Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema kuwa wamejitokeza wananchi wengi ambao kwa hiyari yao wamekubali kuondoka kwenye eneo la Ngorongoro na kwenda Handeni lakini kwa siku ya leo Juni 16 ,2022 zimeanza kuondoka kaya 20 na wiki ijayo zitaondoka kaya nyingine kwa kufuata Sheria , kanuni na taratibu zote za nchi na katika mchakato huo hakuna mtu yoyote ambaye ameshurutishwa au kulazimishwa kuondoka.

Akizungumza leo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Mhe, Mwalimu Raymond Mangwala kumkubidhi Wananchi hao kwa Mkuu wa Mkoa Mkoa wa Arusha kama sehemu ya kuagana rasmi, Mongella amesema anamshukuru Mungu kwa kuiona siku ya leo ya kihistoria.

"Siku hii itakuwa ni leo tu zingine zitakuwa tofauti.Pili nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani yake na sisi kwa umoja wetu kutuamini viongozi wa Mkoa,Wilaya ya Ngorongoro, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, viongozi wote wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha, viongozi wa Serikali na wa kisiasa.

"Viongozi wa kimila na jamii nzima na nisiwasahau kabisa wanahabari tusiposema kwamba kwa baraka za Rais leo tunaweka historia hii tutakuwa hatundeki haki lazima tumshukuru sana kwa hilo.Niwashukuru sana wananchi kwa ujumla wao wote, hawa ndugu zetu leo wanaondoka na wale ambao bado lakini wamejiandikisha na ambao hawajajiandikisha wote wanamchango wao kwenye kufanikisha hili.

"Niseme tu Mwenyezi Mungu katubariki hili limefanikiwa na mnajua wengine hatujakaa muda mrefu ni kama mwaka mmoja na ushee lakini jambo hili lina miaka mingi na mjadala wake ni wa miaka mingi, kuna mafaili na mafaili yamejaa, kila aina ya ushauri wa kitalaaam na wakawaida umetolewa mpaka leo tumefika hapa,"amesema Mongella .

Ameongeza kwamba "Niseme zoezi hili la Wananchi wa Ngorongoro kwa fursa hii iliyotolewa na Serikali ambayo wana hiyari na kwa dhamira zao za dhati binafsi na kwa familia zao.Je Kuna mtu kasukumwa au kalazimishwa? Kama Kuna mtu kalazimishwa au kashurutishwa basi aseme.

"Kwa sababu Rais Samia Hassan katika muongozo wake kila siku kwa viongozi na watendaji wa Serikali lisifanyike jambo lolote la shuruti, kusukuma, la lazima na wananchi lazima waelewe chema ambacho Serikali inawatakia, kwa hiyo naomba ieleweke kwasababu kuna upotoshaji mkubwa unatokea.

"Kuna neno linatumika la Kingereza na wakati mwingine linatumika ili kuficha maana ya lile neno ,kuna neno linatumika linaitwa 'EVICTION' ambayo yake ni kuondolewa .Tafsiri yake sio sahihi kutumika katika zoezi hili,nadhani tutumie tafsiri ya Kiswahili haya maneno mengine yatatupotosha hakuna kuondolewa hapa,"amesema Mongella.

Amefafanua kwasababu kila mtu anatoka kwa hiyari na kwa ridhaa na ambao wamejiandikisha wapo takribani kaya 290 na wameanza na kaya 20 .Wiki ijayo kuna wengine wataondoka, Serikali imeelekeza lazima uondokaji wao uwe wa staha, kibinadamu na heshima inayostahili kwa mujibu wa Sheria ya nchi yetu.

"Na ndio maana hata mchakato wenyewe wa kuondoka inabidi tuupeleke kwa utaratibu na kufuaa Sheria zote za nchi na mimi nataka kusema Kuna mtu amenyanyasika aseme.Na sisi tunaahidi tutafuata Sheria , taratibu na haki zote ambazo nwananchi anastahili na yoyote yule ambaye ataonekana kutaka kwenda Kinyume tutamshughulikia kwa mujibu wa Sheria na taratibu hizo hizo za nchi yetu.

"Tumekuwa na mawasiliano na wenzetu wa Mkoa wa Tanga na nimshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima, uongozi wa Wilaya ya Handeni na mifumo yote pale Msomela na bila kuwasahau viongozi wa Kata ya Misima kule Handeni wamefanya kazi kubwa toka siku ya kwanza.

"Mkuu wa Mkoa yuko Handeni, Waziri wa Maliasili na Utalii yuko Handeni, Waziri wa TAMISEMI Bashungwa yuko Handeni.Leo hawa ndugu zetu wanaenda kukabidhiwa ardhi na makazi huku hifadhani ya Ngorongoro walikuwa hawawezi kuweka makazi ya kudumu, makazi bora kwa viwango vya Sasa.

"Wamesomesha Watoto kwa fursa zilizotolewa na Serikali, hivyo mimi niseme jambo hili ni kubwa na wote tuungane kumshukuru Rais , Serikali ya Awamu ya Sita, tumshukuru Mungu kwa baraka zake, tuungane mkono kwenye mambo makubwa ya kimaendeleo.Na uzuri wa nchi yetu umetoa uhuru wa kikatiba kila mtu kusema anachowaza .

" Huwezi kuwabeza sana wanaopotosha lakini sio uungwana kwenye mambo ya msingi yanayohusu maisha ya watu wetu kuona watu wakipotosha.Wote unajua faida za uhifadhi, Rais anafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha anamgusa kila mwananchi katika kuleta maendeleo, tuna kila sababu ya kumuunga mkono,"amesema Mongella wakati wakiwaaga wakazi wa Ngorongoro ambao wameamua kwa hiyari yao kuondoka.





Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe,John Mongera akizungumza jambo wakati akiagana na jumla ya kaya 20 kati ya 290 zilizoamua kuondoka leo kwa hiyari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambazo zinasafirishwa na serikali katika awamu ya Kwanza kuelekea Msomera,Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga kwa ajili ya kuanza makazi mapya ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo, zoezi hili ni endelevu la kuwasafirisha ambapo serikali itaendelea kuratibu kuhakikisha wanasafirishwa wao pamoja na mali zao.


Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella, aliyeongoza zoezi la kuwapa hundi za fidia wakazi waliokuwa wanaishi Ngorongoro baada kuamua kuanza kuondoka kwa hiyari yao kuelekea Kijiji Cha Msomela wilayani Handeni Mkoa wa Tanga ikiwa ni hatua ya kuunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuwaomba kupisha eneo la hifadji ya Ngorongoro kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania na Dunia kwa ujumla.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-NGORONGORO












Baadhi yao Wakiga





Baadhi ya Magari yakiwa yamebeba jumla ya kaya 20 kati ya 290 zilizoamua kuondoka kwa hiyari katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambazo zinasafirishwa na Serikali katika awamu ya kwanza kuelekea Msomera,Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga kwa ajili ya kuanza makazi mapya ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo,zoezi hili ni endelevu la kuwasafirisha ambapo serikali itaendelea kuratibu kuhakikisha wanasafirishwa wao pamoja na mali zao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments