Bunge Laahirishwa Sababu Makamba Na Naibu Wake Kutokuwepo Bungeni

Mwenyekiti wa Bunge, David Kihenzile leo Alhamisi Juni 2, 2022 ameahirisha shughuli za bunge kwa muda wa dakika 30 kwa sababu Waziri wa Nishati, January Makamba na naibu wake, Stephen Byabato hawapo katika ukumbi wa Bunge wakati mjadala wa hotuba ya wizara hiyo ukitaka kuanza.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni leo wabunge walianza kuchangia hotuba ya Wizara hiyo kwa bajeti ya mwaka 2022/23.

Hata hivyo baada ya Kihenzile kumuita mchangiaji wa kwanza Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige, Waziri Januari Makamba na Naibu wake Stephen Byabato hawakuwepo ndani ya ukumbi wa bunge.

Mmoja wa wabunge ambaye hakupewa nafasi alisikika akiomba mwongozo wa Spika kwa sauti huku Magige akiendelea na mchango ndipo akasema Waziri na Naibu hawapo ukumbini.

Mwenyekiti wa bunge alitaka mjadala uendelee kwa madai kuwa Serikali ipo bungeni lakini wabunge walianza kuguna kwa sauti.

Spika wa bunge ambaye aliongoza kipindi cha maswali na kumpisha Mwenyekiti, alilazimika kurudi na kunong'ona na Kihenzile kwenye kiti kisha akaondoka.

"Waheshimiwa wabunge, naahirisha shughuli za bunge kwa nusu saa hadi Waziri na Naibu wake watakapoingia ukumbini," amesema Kihenzile na kupigiwa makofi.

Hata hivyo wakati wabunge wanatoka Waziri aliingia haraka na kuketi kitini kisha baadhi ya wabunge wakitaka shughuli ziendelee lakini haikuwa hivyo hadi muda waliotangaziwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments