Jinsi Serikali Itakavyookoa Matumizi ya Sh500 Bilioni.

Katika mkakati wa kubana matumizi, Serikali inatarajia kudhibiti mambo kadhaa ikiwemo ununuzi na matumizi ya magari.

Hayo amebainisha  jana Jumanne Juni 14, 2022 bungeni mjini  Dodoma wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23.

Katika hotuba yake hiyo, Dk Mwigulu amesema watadhibiti matumizi hayo kwa kuzingatia waraka wa rais namba moja wa mwaka 1998 kuhusu hatua za kubana matumizi ya serikali na waraka wa mkuu wa utumishi wa umma namba mbili  wa mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia usafiri huo.

“Baadhi ya maeneo yenye gharama kubwa sana kwa serikali ni ununuzi wa magari,  mafuta ya uendeshaji,  vipuri na matengenezo,” amesema.

Amesema serikali inapanga kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu hivyo  lazima matumizi ya umma na ya watumishi  wote yaakisi ugumu wa maisha wanayopitia wananchi  kufuatia athari za Uviko-19 ili fedha zinazopatikana zifanye mambo muhimu.

“Hatua za muda mfupi zitakazochukuliwa ni kupunguza safari za ndani na nje, kukata fedha za ununuzi usio wa lazima, kupunguza ukubwa wa uwakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje, na tutapimiana mafuta ya magari ya Serikali kila mwezi kufuatana na shughuli za lazima,” amesema

Wabunge na BOT watajwa

Katika maelezo yake, Dk Mwigulu amesema utaratibu huo unatumika kwa wabunge na hawajaacha kufanya shughuli majimboni mwao.

"BOT (Benki Kuu) wanapimiwa, baadhi ya taasisi za UN (Umoja wa Mataifa) wanapimiwa. Namwelekeza mlipaji mkuu wa serikali afanye uchambuzi wa wastani wa mahitaji ya mafuta kufuatana na aina ya majukumu, ulazima wa majukumu na ngazi katika utumishi," amesema.

Hatua zaidi

Amebainisha kuwa kwa upande wa hatua za muda wa kati na muda mrefu, anapendekezwa Serikali kubadili kabisa utaratibu uliopo kwa kuwakopesha magari watumishi wenye hadhi ya kuwa na gari la serikali wawe na magari yao wenyewe na wafanye matengenezo wenyewe.

"Wanunue vipuri wenyewe na masuala ya mafuta yaangaliwe kwa utaratibu utakaoonekana unafaa. Kwa sasa Serikali ina magari zaidi ya 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 na inatumia zaidi ya Sh558.45 bilioni  kwa ajili ya ununuzi wa magari,  mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo ambapo kwa sasa ni zaidi ya Sh500 bilioni,”amesema.

Amesema ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo kwa sasa ni zaidi ya Sh500 bilioni kwa mwaka.

Safari za mabosi na madereva

Ameeleza kuwa ukiondoa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mahakama, upande wa serikali wanabaki viongozi wakuu wa wizara, mashirika, wakala, mikoa, wilaya na miradi ambao wasimamizi watakuwa eneo la mradi muda mwingi na kwamba  kwenye makundi haya hawatazidi watano kwa taasisi na wengine wote wenye stahili ya gari la serikali wakopeshwe.

“Tutaondoa utaratibu uliozoeleka, dereva na gari inapitishwa chini bosi anapanda ndege mpaka Mwanza au Mbeya kutoka Dar es Salaam na kurudi hivyo hivyo. Kuna utafiti wa siri ulifanywa, kwa siku moja yalibainika magari ya Serikali yaliyotoka Dodoma kwenda Dar es Salaam yalikuwa 132, na yaliyokuwa yanatoka Dar es Salaam yakipishana kuja Dodoma yalikuwa 76 na mengine nane yalikuwa yamepinduka,” amesema.

Amesema utaratibu huo gharama za matumizi ya magari serikalini zitakuwa zimeokolewa  Sh500 bilioni ambazo zitaelekezwa  kwenye ununuzi wa dawa muhimu hospitali,  kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati na kutekeleza miradi ya maendeleo."

“Tumezidi kupenda ubosi magari makubwa kwa kila mtu serikalini, matumizi ya starehe wakati katika nchi yetu bado kuna watu wanapata shida kupata mlo mmoja," amesema.

Ameongeza kuwa serikali itaachana na mfumo wa sasa wa ununuzi wa umma  ambao umeshindwa kuleta tija kwa kuwa msingi wake mkubwa ni ulinganishaji wa zabuni zilizofunguliwa badala ya bei za bidhaa na huduma ambazo tunazijua.

“Mara nyingi bei hizi za ununuzi zimekuwa kubwa kuliko zile zilizopo sokoni kwa jumla na hata rejareja  na ingekuwa tunanunua kwa ajili ya nyumbani kwetu au kwa ajili ya kampuni zetu tusingekubali bei hizo,” amesema.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments