Jinsi Vibanda Umiza Vinavyowaumiza Watoto

Huenda takwimu za ulawiti na ubakaji zikaongezeka nchini baada ya uchunguzi wa Mwananchi kubaini vichocheo vya matukio hayo kwa watoto, ikiwamo uuzaji, usambazaji na uonyeshaji wa picha chafu katika vibanda vya kuonyeshea video maarufu vibandaumiza.

Hali hiyo inaakisi tukio la mtoto wa miaka 14 aliyetiwa mbaroni kwa tuhuma za kuwalawiti wenzake 19 mkoani Iringa, huku Kamanda wa Polisi mkoa huo, Allan Bukumbi akidai watoto hao walikuwa wakikutana kwenye kibandaumiza kilicho katika eneo la Kihesa Kilolo.

Uchunguzi umebaini zaidi ya asilimia 70 ya maktaba za kuuza video mitaani zinapakua na kuuza picha chafu huku wateja wakubwa wakiwa watoto wanaotumia flashi kutazama nyumbani.

Imebainika kuwa pia picha hizo zinazosambazwa kwa santuri (CD) zinauzwa wastani wa Sh1,000 na wengine wakiuza kwa mafungu ya video walizopakua mtandaoni.

Baadhi ya wauzaji wamekiri kusambaza picha hizo ili kujitafutia fedha.

Katika mabanda hayo, majina yanayotumika kutambulisha kwa watazamaji wa picha hizo chafu ni pamoja na ‘wali nazi, kitonga, awotee, muwekee kwa anayependa na kishoka.’

Nyingine ni pilau, chachandu na kwa kutumia jina la mcheza filamu wa zamani, Rambo.

Miongoni mwa athari ni pamoja na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari (jina tunalihifadhi) kuthibitika akiwa na mchezo wa kuwalawiti vijana wawili wa kidato cha pili.

“Huyo mwanafunzi alikiri kuwa na tabia za kuwalawiti wenzake, nilizungumza na walimu, tumekubaliana waongeze matroni (msimamizi wa malezi) lakini nimefunga vibandaumiza vyote vya picha mtaani kwangu, nimebakiza vya mpira tu,” alisema Mwenyekiti wa Mtaa wa Rwanga, Lukresia Msuya.

Athari hizo zimeanza kutengenezwa ndani ya familia, baadhi ya watoto kutazama nyumbani kwa kutumia flashi wanazonunulia picha hizo chafu mtaani.

Tukio la siku chache zilizopita eneo la Pandia, Mtaa wa Malapa, Ilala linahusisha kunaswa mtoto umri kati ya miaka 4-7 aliyekuwa akiwaingilia watoto chini ya miaka miwili. “Nilipata taarifa za tukio hilo, inawezekana alikuwa anaangalia simu za wakubwa,” alisema mjumbe wa mtaa huo, Khamis Mgwami.


Mitaani

Katika vibandaumiza sita kati ya 20 sugu Mtaa wa Kigogo Kati, Manispaa ya Kinondoni vilibainika kujihusisha na uonyeshaji wa picha hizo chafu, huku mwenyekiti wa mtaa huo, Rashid Luoga akikiri hali hiyo kuwa tishio kwa wanafunzi wengi wa Shule za Msingi Kigogo na Mkwawa.

Luoga, aliyedai kupokea baadhi ya kesi za ulawiti ofisini kwake aliwatupia lawama wanaoendesha shughuli katika mabanda hayo.

“Sina takwimu kwa sasa, lakini tatizo kubwa linaanzia wauzaji wa picha chafu, nina kikosi cha vijana sita wa kufuatilia, tumekuwa tukifuatilia ili kudhibiti lakini wachache wanaendelea,” alisema.

Changamoto hiyo pia imeonekana katika Serikali za Mtaa wa Malapa, Manispaa ya Ilala, mwenyekiti wake Mariam Tuli alidai kufuta kibandaumiza kimoja kilichokuwa kikijihusisha na picha hizo.

“Hilo banda tulizuia wasifungue tena baada ya kubaini watoto wanatoroka shule na kuingia huko,” alisema Tuli.

“Kuna kibandaumiza kingine kinaitwa Bastula tukatoa onyo wakabadilika, tuna vijana wetu wa doria mara kadhaa sasa inawezekana wanafanya kwa siri, lakini ni kweli hali imekuwa mbaya sana kwa sasa.”

Katika kufuatilia mabanda hayo, mwandishi alipata mwenyeji aitwaye Ibrahim Juma aliyeelekeza kuwepo kwa mabanda katika Mtaa wa Kinondoni Shamba.

Mabanda mawili kati ya matano Mwananchi ilibaini huonyesha picha chafu, lakini baadhi yao walikiri kuachana na picha hizo.

Baadhi ya wamiliki wa mabanda hayo mitaa ya Kinondoni, Tandale na Buguruni walidai kuachana na biashara hiyo huku wengine wakikiri kuonyesha huku wakidai kuwa makini na watoto.

“Sionyeshi tena, watu wanatazama mizigo kwenye simu, wateja wamekuwa wachache,” alisema Bozen Emmanueli wa bandaumiza la Mchina, Mtaa wa Kinondoni Shamba anayefunga saa 5:00 usiku.

Mazingira ya kusambaa picha hizo chafu yamechagiza matukio ya ulawiti hadi katika maeneo ya vibanda vya michezo ya game, eneo la Mtaa wa Kombo, Vigunguti jijini hapo wiki kadhaa zilizopita.

“Watoto zaidi ya wanne walikuwa kwenye game, unalipia Sh200, sasa mmoja alipoteza mchezo mmoja na akatakiwa kulipia ila akakosa, ikabidi wakubaliane mmoja alipe deni kisha amwingilie kwa nyuma, kweli akamuingilia mule kwenye banda,” alieleza mmoja kati ya vijana walioshuhudia tukio hilo.

Mwenyekiti mtaa huo, Emmanuel Maranyingi licha ya kutokuwa na taarifa za tukio hilo, alikiri changamoto ya kuonekana wanafunzi wengi katika maeneo hayo wakati wa masomo.

“Huwa tunafanya ukaguzi na vijana wa sungusungu katika mabanda hayo ili kudhibiti athari, tunashukuru sana vijana wa Basata wanaotoa elimu ya kuzuia picha hizo chafu,” alisema Maranyingi.


Ripoti ya Polisi

Wakati hali hiyo ikijitokeza, ripoti ya Jeshi la Polisi kwa mwaka huu inaonyesha matukio ya ukatili wa watoto yaliyoripotiwa yamepungua kutoka 15,870 mwaka 2020 hadi 11,499 mwaka 2021, huku asilimia 89 ya ukatili huo ukihusisha vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Takwimu hizo zilizotajwa katika ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa mwaka 2021, zinaonyesha kuna matukio ya ukatili 7,388 mwaka 2020 ikilinganishwa na matukio 5,803 mwaka 2015.

Baadhi ya viongozi wameonyesha juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo, akiwamo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mafuriko, Ally Mshauri anayetumia Kamati maalumu ya Mtapua kwa ajili ya kukabiliana na viashiria vinavyotishia ongezeko la matukio ya ukatili na ulawiti kwa watoto mtaani humo.

“Mimi kila banda huwa ninaamua kutembelea kimya kimya, ili kujiridhisha maudhui wanayoonyesha. Kwa hiyo nimefanikiwa kukabiliana na changamoto,” alisema Mshauri.


Uzalishaji, masoko

Hata hivyo, baadhi ya walionaswa kwa ushahidi walisema biashara hiyo haina kiwango maalumu cha kununua.

“Mtu akija na pesa yoyote kuanzia Sh100 au Sh500 nampatia video mbili au tatu kulingana na pesa yake,” alisema mmoja kati ya wauzaji katika Mtaa wa Ulongoni B, Kata ya Gongo la Mboto.

Wauzaji wa picha hizo kwa sasa hutumia mfumo wa Virtual Private Network (VPN) ili kuzipakua kwenye mtandao kwa ajili ya wateja wanaohitaji. Mfumo huo huwezesha watu kufikia huduma za intaneti kutoka nchi nyingine na imekuwa ikitumiwa katika baadhi za nchi zinazokabiliwa na zuio hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari alisema kitendo hicho cha matumizi ya njia hizo kurejesha picha chafu kwenye jamii ni kosa kisheria.

“Tulitumia utaalamu wetu tukaondoa uwezekano wa kupakua hizo picha kwa browser (kivinjari). Sasa wao wanaingia huko kwa njia nyingine, ni kosa kama ilivyo kosa la kununua silaha na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 inazuia usambazaji wa picha hizo,” alisema Bakari.

Agosti mwaka jana mamlaka hiyo ilifungia tovuti zote za ngono nchini kwa lengo la kupunguza athari kwenye jamii, hatua iliyoungwa mkono na makundi mbalimbali wakisema hatua hiyo itasaidia kupunguza ulevi wa kutazama picha hizo zinazochochea zaidi vitendo vya ubakaji na ulawiti.

“Nashauri wazuie na VPN kabisa kama inawezekana,” alisema Bob Dere katika mtandao wa Jamii Forum huku Kenzy akisema kisaikolojia ni ulevi mbaya sana unaowafanya watu wajifunze michezo michafu.


Hatari ya dunia

Vyanzo vya habari vinaeleza hivi karibuni, YouTube iliondoa zaidi ya video 120,000 zilizoonyesha unyanyasaji na ushirikishaji wa watoto kingono, huku mwaka 2014 Serikali ya Uganda ikipitisha Sheria ya kuzuia usambazaji wa picha za ngono kwa lengo la kuwanusuru watoto na wanawake.

Katika hali ya kushangaza, mwaka 2015 Serikali ya India iliruhusu mitandao ya filamu za ngono 857 kuwepo baada ya shinikizo kutoka kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian lilizozungumzia ukubwa wa biashara ya video za ngono duniani, mapato ya mwaka ya uzalishaji wa video za ngono kwa sasa yanakadiriwa kufikia Dola 15 bilioni za Marekani (Sh34.5 trilioni), juu ya Netflix Dola 11.7 bilioni (Sh26.9 trilioni) na Hollywood Dola 11.1 bilioni (Sh25.5 trilioni).

Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Mtandao wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Joshua Mwangasa alikiri athari hizo za kidunia, huku akishauri jamii kutoa ushirikiano katika kudhibiti changamoto hiyo.

Mwangasa alisema matumaini yameanza kuonekana baada ya mataifa mbalimbali duniani chini ya Umoja wa Mataifa (UN) kushiriki mkutano wa Cyber Conversion, Vienna nchini Austria ili kuweka misingi ya kunusuru athari za mitandaoni, ikiwamo kudhibiti usambazaji wa video chafu.

“Ulikuwa mkutano wa siku 19, mwaka huu tulijadili kwa nini tusikubaliane kudhibiti athari hizo, tulijadili mifumo ya kitaifa na mambo mengine, kwa hiyo bado majadiliano hayo yanaendelea na mwakani tutakuwa na mkutano kama huo lakini jamii isaidie kuepuka athari hizo,” alisema Mwangasa.


Tishio la kijamii

Wakati uchunguzi ukibaini hali hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupitia dawati la jinsia linakiri athari ya mabanda hayo.

Mrakibu mwandamizi wa polisi, Leah Mbunda alisema, “matukio ya kulawitiana mengi yanatokea maeneo ya shuleni, tukiwauliza wahusika umejifunza wapi? Wengi wanasema walitazama kwenye mabandaumiza au aliona nyumbani kwa wazazi, tatizo kwenye mabandaumiza wanaonyesha mafichoni”.

Alisema baadhi ya hatua ambazo zimekuwa zikitekelezwa na ofisi yake ni pamoja na utoaji wa elimu katika Serikali za mitaa na kuchukua hatua za kisheria endapo kuna kosa la jinai.

“Lakini polisi kata na wakaguzi kata hutoa elimu katika mabanda hayo kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa.”

Alisema kutokana na mabadilikoa mbalimbali yaliyochagizwa na utandawazi, Sheria ya Makosa ya Jinai inatakiwa kufanyiwa maboresho ya kutambua umri wa watoto wanaotakiwa kuwajibika kisheria.

“Sheria inasema anayeingiliwa au kumuingilia mwenzake chini ya miaka 12 hawawajibiki kisheria, hakuna kesi hapo, ila sasa hivi utandawazi wanapevuka mapema wakiwa na miaka 11 tu na siyo 15-16 ilivyokuwa zamani, kwa hiyo sheria inatakiwa itazamwe eneo hilo,” alisema Mbunda.


Uuzaji, usambazaji

Wakati hali hiyo ikiendelea katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, timu ya vijana wa Chama cha Maktaba za Video Tanzania (TVLA) chini ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) imeendelea na operesheni za mtaa kwa mtaa kukamata na kutoa elimu kwa wauzaji na wasambazaji wa picha hizo chafu tangu mwaka 2016.

Kwa mujibu wa ripoti ya TVLA, kati ya Septemba 2020 hadi Januari mwaka huu, maktaba 1,786 zimefanyiwa ukaguzi katika manispaa tano za jiji hilo.

Kinondoni maktaba 373, Ilala (480), Ubungo (306), Temeke (601) na Kigamboni (26), huku asilimia 70 zikikutwa na biashara ya CD na picha za ngono.

“Hili ni tatizo la kitaifa, hali inazidi kuwa mbaya zaidi, uzoefu unaonyesha kila maktaba tatu kati ya tano zinauza picha hizo mikoani, tunapambana ili wasisambaze zaidi kwenye mabandaumiza au nyumbani ambako vijana hutumia flash kutazama,” alisema Mwenyekiti wa TVLA, Richard Jorams.

Februari 10, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi lilimkamata mwalimu wa mafundisho ya dini Kanisa la Katoliki Mpanda Mjini, Joseph John (27) akituhumiwa kuwalawiti watoto wanne.

Machi 29, mwaka huu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita lilimsaka mkazi wa Nyarugusu kwa tuhuma za kuwalawiti ndugu zake watatu wenye umri wa miaka 10 na mwingine minane.

Martine Lukwandali, Mratibu wa Manispaa ya Ilala na Ubungo kupitia chama hicho alisema zaidi ya mitaa 50 imekiri kwa maandishi kuelemewa na changamoto ya mabanda hayo katika mitaa yao, licha ya elimu kutolewa zaidi ya mara moja. Barua hizo zenye mihuri ya Serikali zilithibitishwa na Mwananchi.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments